1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mamilioni ya Waingereza wapiga kura katika uchaguzi mkuu

4 Julai 2024

Wananchi wa Uingereza Alhamisi wanapiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kukirejesha madarakani chama kikuu cha upinzani cha Labour, na kumaliza takribani muongo mmoja na nusu wa utawala wa chama cha Conservative.

https://p.dw.com/p/4hrBq
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak na mkewe Akshata Murty
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak na mkewe Akshata Murty Picha: Scott Heppell/AP Photo/picture alliance

Huu ni uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu Boris Johnson aliposhinda kwa kishindo kura ya mwaka 2019. Unafanyika baada ya Waziri Mkuu Rishi Sunak kuchukua hatua ya kushangaza ya kuitisha uchaguzi huo miezi sita mapema kuliko ilivyotakiwa.

Zaidi ya vituo 40,000 vya kupigia kura kutumika

Upigaji kura ulianza tangu saa moja kamili asubuhi kwa saa za Uingereza kwenye zaidi ya vituo 40,000 vya kupigia kura nchini kote. Rishi Sunak alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliojitokeza kupiga kura katika jimbo lake la Richmond na Northallerton huko Yorkshire, kaskazini mwa England, akiwa ameongozana na mkewe Akshata Murty.

Baada ya miaka 14 madarakani chini ya mawaziri wakuu watano ndani ya kipindi cha miaka minane, chama cha Sunak cha Conservative kinatarajiwa kushindwa na chama cha Labour kinachoongozwa na Keir Starmer, chenye kufuata siasa za mrengo wa kushoto.

Kibao kinachoonyesha kituo cha kupigia kura Uingereza
Kibao kinachoonyesha kituo cha kupigia kura UingerezaPicha: David Cliff/AP Photo/picture alliance

Starmer amepiga kura katika jimbo la Holborn na St. Pancras, kaskazini ya London, akiwa ameongozana na mkewe Victoria. Chama cha Sunak kimekuwa kikijitahidi kuwahakikishia wapiga kura kuhusu masuala kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na mzozo katika Huduma ya Taifa ya Afya.

Viongozi wawarai wapiga kura

Viongozi wa vyama walitoa wito wao wa mwisho kwa wapiga kura baada ya kuzunguka nchi yote tangu uchaguzi ulipotangazwa. Waziri Mkuu Sunak alisema, siku ya Alhamisi inawakilisha wakati muhimu kwa mustakabali wa nchi, akidai kuwa chama cha Labour kitatumia nguvu zake zisizoweza kudhibitiwa kuongeza kodi ikiwa kitapata wingi wa kura.

Kwa upande wake Starmer amesema Uingereza haiwezi kumudu miaka mitano zaidi chini ya chama cha Conservative, akiongeza kubainisha kuwa Uingereza inaweza kuanza ukurasa mpya chini ya chama chake.

Kwa mujibu wa Starmer, mustakabali wa Uingereza uko kwenye masanduku ya kupigia kura. Utafiti wa maoni ya wapiga kura unaonesha kwamba Starmer atapata ushindi mkubwa kutokana na wapiga kura kuchoshwa na Wahafidhina, ambao wameonesha kiwango cha juu cha mgawanyiko.

Kiongozi wa chama cha Labour, Keir Starmer
Kiongozi wa chama cha Labour, Keir Starmer Picha: Cameron Smith/Getty Images

Akizungumza baada ya kupiga kura kwenye kituo cha Hackney, East London, raia wa kawaida Ianthe Jacob, amesema amerejea kutoka Australia hivi karibuni na amegundua kwamba kila kitu kimebadilika na hakiendi sawa nchini humo na watu wengi hawaridhishwi.

''Nadhani ni jambo muhimu kubadilisha serikali na bila kujali ushawishi wako wa kisiasa, ukweli kwamba serikali mpya itakuwa na nafasi ya kufikiria juu ya kile wanachotaka kufanya, na bila kuwa na shinikizo. Nadhani ni bora kwa njia hiyo,'' alifafanua Jacob.

Soma zaidi: Chama cha Labour chatabiriwa kukishinda chama cha Conservative

Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa nne usiku kwa saa za Uingereza, na matokeo ya awali yatatangazwa kuonyesha mwelekeo halisi wa matokeo ya vyama vikuu katika ngazi ya kitaifa. Matokeo ya majimbo 650 ya ubunge nchini Uingereza yataanza kuingia usiku kucha, huku chama kilichoshinda kikitarajiwa kupata viti 326, kiwango kinachotakiwa kwa ajili ya kuwa na wingi wa wabunge, ifikapo mapema Ijumaa asubuhi.

(DPA, AFP, AP, Reuters)