1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU, Korea Kusini zaikosoa Urusi, Korea Kaskazini

22 Mei 2023

Korea Kusini na Umoja wa Ulaya zimekubaliana leo kuimarisha ushirikiano juu ya usalama katikati mwa mzozo wa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na vitisho vya nyuklia kutoka Korea Kaskazini.

https://p.dw.com/p/4RfxG
Südkorea | Ursula von der Leyen und Charles Michel in Seoul
Picha: Jung Yeon-Je/REUTERS

Kwenye mazungumzo ya Jumatatu yalioadhimisha miaka 60 ya uhusiano kati ya pande mbili, rais Yoon na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika tamko lao la pamoja wamelaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine wakiutaja kama ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa.

Pia wamekosoa juhudi zinazoendelea za Korea Kaskazini kuongeza shehena yake ya silaha za nyuklia, na vitisho vya Pyongyang juu ya uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Korea Kusini.

Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol alikutana na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen mjini Seoul baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa mwishoni mwa juma wa Kundi la Mataifa Saba yanayoongoza kiviwanda mjini Hiroshima, Japan.

Südkorea | Ursula von der Leyen und Charles Michel in Seoul
Viongozi wa Umoja wa Ulaya, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen (wa pili kutoka kushoto), na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel (wa pili kutoka kulia) wakitembelea makaburi ya taifa mjini Seoul Mei 22, 2023.Picha: Yonhap/picture alliance

"Tunakubaliana kudumisha na kuongeza shinikizo la pamoja kwa Urusi, haswa kupitia utekelezaji mzuri wa hatua zinazozuia," walisema katika taarifa ya pamoja. "Tumejitolea kuunga mkono ufufuaji na ujenzi wa Ukraine na tunasalia na azma ya kuiunga mkono Ukraine kwa muda mrefu kadri itakavyohitajika."

Soma pia:Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aitaka Korea Kaskazini kusitisha majaribio ya makombora ya nyuklia

Yoon amekuwa akisisitiza juu ya kuwepo kwa uhusiano mkubwa wa kiusalama na Ulaya na washirika wengine wa Marekani ili kushughulikia changamoto za kimataifa, ikiwa ni pamoja na mzozo wa Ukraine na mvutano kuhusu msimamo wa China kuelekea Taiwan.

Malengo ya nyuklia ya Korea Kaskazini

Pia anataka ushirikiano ili kuzuia malengo ya nyuklia ya Korea Kaskazini. Mnamo mwezi Juni mwaka jana, alihudhuria mkutano wa kilele wa NATO kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa Korea Kusini.

Katika mazungumzo ya Jumatatu, Yoon na viongozi wa Umoja wa Ulaya wamelaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, na pia harakati za Pyongyanga kutengeneza silaha za nyuklia pamoja na vitisho vyake dhidi ya Korea Kusini.

Michel alisema kuendelea kwa mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine kunaonyesha kwamba ushirikiano wa kina kati ya EU na Korea Kusini "sio anasa. Ni jambo la lazima."

Viongozi hao watatu waliitaka Korea Kaskazini kusitisha vitendo vinavyoibua mvutano wa kijeshi na kurejea kwenye mazungumzo ya kutokomeza silaha za nyuklia.

Korea Kaskazini yafyatua tena makombora

"Umoja wa Ulaya hautakubali kamwe (Korea Kaskazini) kumiliki silaha za nyuklia kama hali ya kawaida ya mambo, kama ambavyo hatukubali uchokozi wa kijeshi wa Urusi dhidi ya Ukraine," von der Leyen alisema katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari.

Yoon alisema viongozi hao watatu walitambua kuwa mipango ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini ni tishio linalokwenda mbali ya Rasi ya Korea.

Korea Kaskazini imerusha takriban makombora 100 tangu kuanza kwa 2022, mengi yake yakiwa ya nyuklia ambayo yanaliweka bara la Amerika na Korea Kusini ndani ya umbali wa kushambulia.

Soma pia: Viongozi wa Kundi la Nchi saba tajiri duniani wanakusudia kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusi

Wataalamu wanasema Korea Kaskazini inaamini kwamba hifadhi yake ya silaha iliyopanuliwa itaisaidia kulaazimisha muafaka kutoka kwa wapinzani wake.

G7 yalaani uvamizi wa Urusi, Korea Kaskazini

Kwenye mkutano wa G7, viongozi wa Japan, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Canada na Italia pamoja na Umoja wa Ulaya walilaani uvamizi wa Urusi na kusisitiza uungaji mkono wao kwa Ukraine.

Waliitaka Korea Kaskazini kujiepusha na vitendo vyovyote vya kudhoofisha au kuzidisha hali hiyo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alikutana na baadhi ya waungaji mkono wake wakubwa wakati mkutano wa kilele wa G7 uliofungwa Jumapili, na kuongeza kasi ya juhudi za vita vya nchi yake licha ya Urusi kudai ushindi katika uwanja wa vita ambao ulipingwa haraka na Ukraine.

Hatimaye Trump akutana ana kwa ana na Kim

Hata kabla ya Zelenskyy kutua Jumamosi, mataifa ya G7 yalikuwa yametangaza vikwazo vipya na hatua nyingine zilizokusudiwa kuiadhibu Moscow kutokana na uvamizi wake ulioanza Februari mwaka jana.

Yoon pia alikutana na Zelenskiy pembezoni mwa mkutano wa G7 na kuahidi kutuma vifaa vya kutegua mabomu, magari ya wagonjwa na vitu vingine.

Ushirikiano mwingine

Katika masuala mengine ya kimataifa, pande hizo zimekubaliana kuunda kile walichokiita ushirikiano wa kijani, kuchochea mabadiliko ya kirafiki, huku viongozi hao wakionya kwamba mgogoro wa ncha tatu unaoikabili sayari yetu wa mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa viumbe hai na uchafuzi wa mazingira unatishia uwepo wa sayari hiyo.

Pande zote mbili pia zimeafikiana kuimarisha ushirikiano wa afya, ambapo watafanya kazi pamoja kutambua na kukabiliana na vitisho vya afya, na kusaidia nchi nyingine kuzuia na kukabiliana na vitisho hivyo.

Chanzo: Mashirika