1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mataifa ya G7 yakusudia kuiongezea Urusi vikwazo zaidi

15 Mei 2023

Viongozi wa nchi saba tajiri duniani,G7 wakusudia kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusi kwa kuilenga sekta ya nishati ya nchi hiyo na mauzo ya nje ambazo wanasema biashara hizo ndio zinaipa Urusi nguvu za kijeshi.

https://p.dw.com/p/4RLkS
Japan | Treffen der G7 Finanzminister
Picha: Issei Kato/REUTERS

Viongozi hao wa nchi na serikali za mataifa ya G7 wanatarajiwa kukutana kwenye mkutano wa kilele mnamo wiki hii katika jiji la Hiroshima, nchini Japan ambayo ndio mwenyeji wa mkutano huo wa G7. Mkutano huo wa kilele wa viongozi unatarajiwa kuanza tarehe 19 hadi 21 mwezi huu.

Mkutano wa awali wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu wa nchi za G7.
Mkutano wa awali wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu wa nchi za G7.Picha: Issei Kato/REUTERS

Hatua mpya za vikwazo zitaelekezwa kwa nchi zinazokiuka vikwazo vilivyowekwa hadi sasa dhidi ya Urusi. Kwenye mkutano wa kilele, viongozi hao wa nchi saba tajiri watajadili njia za kubana uzalishaji nishati na biashara zinazoipa Urusi nguvu za kijeshi. Hatua hiyo ya viongozi wa G7 dhidi ya Urusi inachukuliwa wakati ambapo washirika wa Ukraine, ambao ni nchi za magharibi wanasaka njia mpya za kuiongezea Urusi vikwazo zaidi mbali na vile vya kudhibiti uuzajiji wa bidhaa za nchi hiyo nje ya nchi, vizuizi vya visa na ukomo katika bei ya mafuta.

Yote hayo yamesababisha serikali ya Urusi kukabiliwa na ugumu katika uendeshaji wa shughuli zake lakini hata hivyo Rais wa urusi Vladimir Putin hajaonesha dalili za kuwa tayari kusitisha uvamizi wa nchi yake nchini Ukraine. Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umepindukia mwaka mmoja sasa.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: SPUTNIK via REUTERS

Juu ya urusi kuongezewa vikwazo, Rais wa zamani wa nchi hiyo Dmitry Medvedev, alisema hivi karibuni kwamba hatua hiizo za nchi za magharibi dhidi ya nchi yake zitailazimisha Urusi isimamishe makubaliano juu ya usafirishaji wa ngano ya Ukraine kupitia bahari nyeusi. Uhakika wa upatikanaji wa chakula baada ya vita vya Ukraine pia ni suala lingine muhimu litakalojadiliwa kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi saba tajiri huko nchini Japan.

Mkutano huo wa kilele wa wiki hii utakaohudhuriwa na viongozi wa nchi saba tajiri, G7 katika jiji la Hiroshima nchini Japan utayajumuisha mataifa mengine manane ambayo yamealikwa katika kujaribu kutatua maswala mbalimbali yanayoikabili dunia.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amefahamisha kwamba mataifa hayo yaliyoalikwa ni pamoja na Korea Kusini, Australia, India, Brazili, Vietnam, Indonesia, Comoro na Visiwa vya Cook. Kishida amesema anatumai kukutana nchi hizi mseto kutasaidia katika juhudi za kukabiliana na maswala kama vile kuidhibiti China uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida.
Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida.Picha: Kyodo/REUTERS

Japan pia inataka kuimarisha uhusiano wake na nchi washirika wa Marekani na mataifa yanayoendelea na kupiga hatua katika kushughulikia suala la nyuklia kwa lengo la kuwa na ulimwengu huru usio na silaha za nyuklia, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kutokana na vitisho vya nyuklia kutoka nchi za Korea Kaskazini na Urusi. Kundi la G7 linajumuisha nchi za Marekani, Japan, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza.

Vyanzo: RTRE/AP