1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Katumbi: Tshisekedi ameshindwa kuleta utulivu Kongo

24 Novemba 2023

Mwanasiasa mashuhuri na kinara wa upinzani nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Moise Katumbi katika kampeni zake katika mji wa Goma amemshtumu Rais Felix Tshisekedi kushindwa kumaliza vurugu katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4ZOhU
Wafuasi wa mwanasiasa na mgombea urais Kongo Moise Katumbi
Wafuasi wa mwanasiasa na mgombea urais Kongo Moise KatumbiPicha: JOHN WESSELS/AFP

Baada ya kuzindua kampeni zake za uchaguzi mjini Kisangani na katika mkoa jirani wa Ituri, Katumbi amelaani pia uzembe wa  mamlaka katika kushughulikia hali ya usalama mashariki mwa nchi hiyo .

Akiwa ameandamana na washirika wake wapya, wakiwemo waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo, Seth Kikuni na Frank Diongo, Moise Katumbi alilakiwa na maelfu ya wafuasi ambao hawakuruhusiwa kuingia ndani ya uwanja wa ndege  wa kimataifa mjini Goma kabla ya ndege yake kutua.

Pamoja nakumuunga mkono, raia hao waliokuwa wakibeba  bendera za chama cha Ensembele pour la Republique kinacho ongozwa na tajiri huyo ambaye pia ni Gavana wa zamani  wa jimbo la katanga, walionesha pia hasira yao baada yakuzuiliwa na jeshi polisi kumkaribisha kiongozi wao.

Soma pia:Wagombea sita wa urais kongo waitaka mahakama ya juu kuhakikisha uchaguzi wa haki

Wakati wa mkutano wa hadharani  uliofanyika jana Alhamisi jioni, Moise KATUMBI mgombea wa uchaguzi wa Urais wa desemba 20, aliahidi kurejesha usalama katika mikoa ya Ituri na kivu kaskazini,inayoyumbishwa na vita kwa sasa.

Changamoto ya ajira kwa vijana Kongo

Kwa takriban dakika 60, mgombea huyo ambaye uraia wake unaendelea kuzua utata  nchini Kongo, alikosoa kwa nguvu rekodi ya utawala wa sasa, akilaani kuendelea kwa ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na mishahara duni kwa askari  wanaokabiliana na makundi ya waasi kila uchao.

Vyama vya siasa vya upinzani Afrika vimetekeleza wajibu wao?

Wakati huo huo, kundi jengine la vijana waliandamana upande wa mashariki mwa mji wa Goma wakitaka kuzuiliwa kwa Katumbi kuingia mjini Goma wakimtuhumu kutolitaja taifa la Rwanda kuunga mkono waasi wa M23 katika vita vinavyoendelea sehemu mbalimbali hapa kivu kaskazini.

Soma pia:Kuondolewa vipeperushi vya wagombea kunazusha mvutano Kongo

Hata hivyo, wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea, baadhi ya wagombea urais wanakosoa ukiukwaji wa taratibu  katika mchakato wa uchaguzi.

Wagombea sita ambao ni Martin Fayulu, Floribert Anzuluni, Theodore Ngoy, Nkema Liloo pamoja na Jean-Claude Baende wametishia kuwasilisha malalamiko yao mbele ya mahakama makuu wakimshtaki kiongozi wa tumehuru ya uchaguzi pamoja na waziri wa mambo ya ndan kwa ukiukwaji huo.