1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DR Kongo: Kampeni za uchaguzi mkuu kuanza rasmi 20.11.2023

19 Novemba 2023

Kampeni za uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaanza rasmi Jumatatu tarehe 20.11.2023 na zitaendelea kwa muda wa mwezi mmoja.

https://p.dw.com/p/4Z9AD
DR Kongo vor den Wahlen
Picha: JUSTIN MAKANGARA/REUTERS

Kampeni hizo zinaanza huku kukiwa na hali ya wasiwasi wa hali ya kisiasa nchini humo na mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

Eneo hilo la mashariki mwa Kongo limekumbwa na mapigano kwa miongo mitatu, na ghasia zinaongezeka hasa baada ya kundi la M23, kuteka eneo kubwa la jimbo la Kivu kaskazini hivi karibuni. Kundi hilo linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekediPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Mchambuzi wa maswala ya kisiasa kutoka taasisi ya utafiti ya Ebuteli,Tresor Kibangula amesema dhamira ya kisiasa ya kuendana na kalenda ya uchaguzi ipo, lakini kuna mashaka kutokana na kwamba huenda zoezi hilo likakabiliwa na matatizo ya kiufundi.

Soima:Wagombea urais Kongo wataka kuzuiwa wizi wa kura

Wagombea 26 wanawania wadhfa wa urais na takriban wapiga kura milioni 44 wamejiandikisha kupiga kura, kati ya wakazi karibu milioni 100.

Raia wa Kongo watamchagua rais mnamo, Disemba 20, katika zoezi hilo la kupiga kura. Vilele wapiga kura watawachagua wabunge na wawakilishi wa serikali za mitaa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Tume ya Uchaguzi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Ceni), inapambana kuandaa zoezi la upigaji kura katika eneo la ukubwa wa kilomita za mraba milioni 2.3 lililo na miundombinu isiyo mizuri.

Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2018.
Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2018.Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Kwa jumla wagombea 25,832 wameorodheshwa kugombea katika uchaguzi wa wabunge, wagonbea 44,110 watagombea uwakilishi katika majimbo na wagomea wengine 31,234 wanatafuta nafasi ya kuwakilisha katika mabaraza ya manispaa.

Soma:Mahakama Kuu DRC yatupilia mbali kesi ya kumzuia Katumbi kuwania urais

Kampeni za awali zimekuwa zikiendelea kwa muda, huku Rais Felix Tshisekedi, anayewania muhula wa pili, akihudhuria hafla nyingi za umma na washirika wake wakikumbusha na kujivunia utendaji kazi wa rais huyo wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi ambaye anatarajiwa kushinda uchaguzi huo. 

Martin Fayulu mgombea wa upinzani katika kinyang'anyiro cha urais nchini DR Kongo.
Martin Fayulu mgombea wa upinzani katika kinyang'anyiro cha urais nchini DR Kongo.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/picture alliance

Jumatatu tarehe 20.11.2023 ambayo itakuwa siku ya ufunguzi rasmi wa kampeni za uchaguzi mkuu, rais Tshisekedi atahutubia mkutano katika uwanja wa Mashahidi, mjini Kinshasa huku mmoja wa wapinzani wake wakuu, Martin Fayulu, akiwa amepanga kuhutubia mkutano katika mkoa ulio jirani na jiji la Kishansa.

Wagombea wengine wakuu wa upinzani ni Moise Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga, eneo lenye utajiri wa madini na daktari Denis Mukwege,  aliyepokea Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2018.

Soma:Wafuasi wa Katumbi waridhishwa kuruhusiwa kuwania urais DRC

Wawakilishi kutoka vyama vinne kati ya vitano vikuu vya upinzani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walifanya mazungumzo nchini Afrika Kusini wiki hii ili kuunda muungano kabla ya uchaguzi mkuu wa Disemba.

Chama ambacho hakikushiriki ni kile cha Martin Fayulu, kiongozi wa Edice (Engagement for Citizenship and Development), ambaye anadai kuwa ndiye mshindi wa kweli wa uchaguzi wa Desemba mwaka 2018 ambao uliporwa na Rais Felix Tshisekedi.

Moise Katumbi, mmoja wa wagombea wakuu katika uchaguzi wa rais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Moise Katumbi, mmoja wa wagombea wakuu katika uchaguzi wa rais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Wagombea wanne wa upinzani waliowakilishwa mjini Pretoria ni pamoja na Moise Katumbi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Denis Mukwege, waziri mkuu wa zamani Matata Ponyo na mbunge Delly Sesanga.

Chanzo:AFP