1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joshua Kimmich:Nahodha mpya wa timu ya taifa ya Ujerumani

2 Septemba 2024

Joshua Kimmich ameteuliwa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani baada ya Ilkay Gündogan aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kutangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya taifa.

https://p.dw.com/p/4kC2M
 Julian Nagelsmann und Joshua Kimmich
Joshua Kimmich ameteuliwa kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa ya UjerumaniPicha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Joshua Kimmich ameteuliwa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani baada ya Ilkay Gündogan aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kutangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya taifa.

Tangazo la kuteuliwa kwa Kimmich kuwa nahodha wa Die Mannschaft limetolewa leo na kocha mkuu wa Ujerumani Julian Nagelsmann.

Nyota huyo wa Bayern Munich Kimmich ndiye aliyecheza mechi nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote katika timu ya taifa baada ya Gündogan na watangulizi wengine kama Manuel Neuer, Thomas Müller na Toni Kroos ambao kwa sasa si sehemu ya timu ya taifa tena.

Soma zaidi. Nagelsmann atumai Rudiger atakuwa fit kucheza dhidi ya Denmark

Kimmich mwenye umri wa miaka 29, ameichezea Ujerumani mechi 91 tangu aicheze kwa mara ya kwanza mwaka 2016. Kiungo huyo alikuwa nahodha msaidizi katika mashindano ya mataifa ya Ulaya EURO 2024 yaliyoandaliwa Ujerumani hivi majuzi.

Rudiger na Haverts watakuwa wasaidizi

Nagelsmann amesema kwamba beki wa Real Madrid, Antonio Rüdiger na mshambuliaji wa Arsenal Kai Havertz watakuwa manahodha wasaidizi.

Antonio Rüdiger
Antonio Rudiger atakuwa nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya UjerumaniPicha: H. Langer/IMAGO

"Tumepata mchanganyiko mzuri kwa wote watatu," Nagelsmann alisema. "Watakuwa wanawajibika kwa jinsi kikosi kinavyoonekana."

Kocha huyo alikuwa akizungumza wakati Ujerumani ikianza maandalizi ya ligi ya mashindano ya mataifa ya Ulaya ambapo Jumamosi hii wanashuka dimbani dhidi ya Hungary na siku tatu baadaye watakutana na Uholanzi.

Ni mechi za kwanza tangu Ujerumani ilipopoteza dhidi ya Uhispania katika mchezo wa robo fainali ya Euro na pia mwanzo wa maandalizi kuelekea michuano ya Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Mexico na Kanada.