1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gosens: Ndoto ya kucheza Bundesliga imetimia

Josephat Charo
23 Agosti 2023

Mchezaji kiungo raia wa Ujerumani Robin Gosens amesema ndoto yake ya muda mrefu ya kucheza katika ligi kuu ya kandanda ya Ujeruamni Bundesliga imetimia baada ya kuchez mechi yake ya kwanza na klabu yake Union Berlin.

https://p.dw.com/p/4VUy4
Deutschland München | UEFA EURO 2020 | Portugal vs Deutschland | Robin Gosens
Picha: Matthias Hangst/AFP/Getty Images

Kiungo wa Ujerumani Robin Gosens amesema ametimiza ndoto yake katika mechi yake ya kwanza ya Bundesliga na klabu yake mpya ya Union Berlin Jumapili iliyopita. "Mimi ni mchezaji ambaye kwa kawaida huwa sina hofu kabla mechi. Hali ilikuwa tofauti kabla mechi dhidi ya Mainz. Nilishikwa na hofu kidogo, wasiwasi wa furaha." aliwaambia waandishi habari siku ya Jumatano.

Gosens anacheza kwa mwara ya kwanza katika Bundesliga. Mjerumani huyo alianza kucheza soka la kulipwa na timu ya Heracles Almelo nchini Uholanzi, kabla kuhamia nchini Italia ambako alichezea klabu ya Atalanta na Inter Milan.

"Hii si ndoto tu ya kawaida. Kwangu mimi ni moja kati ya ndoto zangu kubwa za tangu utotoni, mojawapo ya malengo yangu ya maisha niliyofanikiwa kuyatimiza," alisema Gosens.

Mazingira katika uwanja pia yalimfurahisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29. "Nimepata bahati kubwa kucheza katika viwanja kadhaa na mazingira ya nchi za nje. Lakini kilichofanyika hapa Jumapili kwa kweli si cha kawaida," alisema. "Mtazamo huu chanya, hisia hizi ambazo baadaye zinahamishiwa uwanjani. Hii inasisimua sana hapa."

Gosens alitangaza Jumanne jioni wiki iliyopita kwamba ameihama klabu yake Inter Milan katika ligi ya Serie A nchini Italia na amejiunga na Union Berlin katika Bundesliga.

Fussball Champions League | Inter Mailand - Bayern München
Kutoka kushoto, Robin Gosens, Marcel Sabitzer na Joshua Kimmich katika pambano la kundi C la ligi ya mabingwa Ulaya kati ya Inter Milan na Bayern Munich katika dimba la Stadio Giuseppe MeazzaPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

"Nimekuwa nikisema mara zote imekuwa ndoto yangu kucheza nchini Ujerumani na katika Bundesliga siku moja. Miaka michache iliyopita ya Union imekuwa ya kuvutia, ungeweza kuona hivyo ugenini," Gosens alisema katika tangazo lililochapishwa kwenye tovuti ya Union.

"Katika mazungumzo na maafisa wa klabu, nilihisi kukubaliwa sana na kuaminiwa, kwa hiyo uamuzi haukuwa mgumu kwangu."

Mkurugenzi Mkuu wa timu ya wanaume ya soka ya Union Berlin, Oliver Ruhnert alisema, "Kwa kumpata Robin, tulifanikiwa kumsajili mchezaji anayeamini na kusimamia kujitolea kwa dhati, fikra na 'morali' wa timu. Ndani na nje ya uwanja, atakuwa na jukumu muhimu la uongozi kwetu."

Maelezo kuhusu mkataba wa Gossens hayakutolewa na klabu hiyo ya mji mkuu, Berlin.

Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani la Bild, Gosens alikuwa mjini Berlin Jumanne wiki iliyopita kufanyiwa vipimo vya afya na kusaini mkataba hadi Juni 2027. Klabu ya Union inasemekana imeilipa Inter Milan kitita cha euro milioni 16.4 kwa uhamisho wake. Kiwango hiki kinamfanya Gossens kuwa mchezaji wa thamani kubwa katika historia ya Union Berlin.

(dpa)