1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harry Kane kuanza katika mechi yake ya kwanza ya Bundesliga

17 Agosti 2023

Kocha wa Bayern Munich amesema mshambuliaji mpya Harry Kane "ameonyesha matokeo mazuri" kwenye kikosi cha timu hiyo na anatarajiwa kuanza mechi yake ya kwanza ya Bundesliga kesho Ijumaa dhidi ya Werder Bremen.

https://p.dw.com/p/4VI35
Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry Kane
Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry KanePicha: Revierfoto/dpa/picture alliance

Thomas Tuchel ameeleza kuwa nyota huyo, ataanza katika mechi ya kesho iwapo "hakuna lolote kubwa litakalotokea” na kwamba nyota huyo ameingiliana vyema na wachezaji wenzake. "Anatuongezea nafasi kubwa ya kushinda mechi ya kesho. Ingawa hatutashinda kila mechi, lakini nina uhakika wa asilimia 100 na uwezo wake. Kufanya kazi na Harry Kane kila siku kumenithibitishia hilo."

Saa chache baada ya kutangazwa kuwa mchezaji mpya wa Bayern, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uingereza aliingia kama mchezaji wa akiba kunako dakika ya 64 ya mchezo katika fainali ya Kombe la Super Cup dhidi ya RB Leipzig waliopoteza kwa mabao 3-0 Jumamosi iliyopita.

Kane amesema kuwa huenda akahitaji muda wa kuizoea Bayern Munich baada ya kujiunga nao katika dirisha la uhamisho la msimu wa joto akitokea Tottenham Hotspurs inayoshiriki Ligi Kuu ya Premia.

Mshambuliaji huyo ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji katika timu ya taifa ya England na Tottenham Hotspurs anatarajiwa kujaza pengo la safu ya ushambuliaji lililoachwa wazi na Robert Lewandowski aliyejiunga na Barcelona.