1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wamimina sifa kwa Rais Joe Biden

22 Julai 2024

Salamu za pongezi kutoka maeneo mbalimbali duniani zinaendelea kumimika baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais.

https://p.dw.com/p/4iaLA
USA Wahlen Präsident Joe Biden
Picha: Matt Rourke/AP Photo/picture alliance

Pongezi hizo zimetolewa na viongozi mbalimbali akiwemo Kansela waUjerumani Olaf Scholz ambaye amesema anampongeza rafiki yake Joe Biden kwa mengi aliyoyafanikisha kwa nchi yake, kwa Ulaya, na kwa ulimwengu mzima. Kansela wa Ujerumani ameserma uamuzi wa Biden wa kutogombea urais unastahili kuheshimiwa.

Ujerumani Berlin | Kansela Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Ralf Hirschberger/AFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock pia ameupongeza uamuzi wa Rais Joe Biden wa kusitisha kampeni zake na kujitoa kwenye uchaguzi wa Rais. Amesema anauheshimu sana uamuzi wa rais wa Marekani Joe Biden, aliyeweka maslahi ya nchi yake mbele kuliko maslahi yake binafsi.

Soma Pia: Netanyahu aanza ziara nchini Marekani 

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amemsifu Biden kwa kuchukua maamuzi mengi magumu wakati wa utawala wake ambayo yameleta usalama zaidi kati nchi yake Poland, Marekani pamoja na demokrasia kuimarika ulimwenguni.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, ambaye Biden alihudumu kwa mihula miwili kama makamu wake wa rais amesifu utendaji kazi wa kiongozi huyo.

Rais wa zamani wa Marekani Obama
Rais wa zamani wa Marekani Barack ObamaPicha: Jane Barlow/PA Wire/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, amesema anauheshimu uamuzi wa Biden na kwamba anaamini kuwa Biden amefanya uamuzi wake kulingana na kile anachokiamini kuwa ni bora kwa watu wa Marekani.

Salamu za pongezi kwa Joe Biden pia zimetolewa na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida aliyesema huo ni uamuzi bora wa kisiasa.

Soma Pia: Baada ya Biden kujiengua, Kamala Harris aanza kuupigania urais

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amemshukuru Biden kwa uungaji wake mkono usioyumba kwa Israeli wakati wote.

Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese, amemshukuru Biden kwa uongozi wake. Amesema nchi hizo mbili chini ya urais wa Joe Biden zilizingatia dhamira yao ya pamoja kwa ajili ya maadili ya demokrasia, usalama, ustawi wa kiuchumi na hatua za kukabiliana na hali mbaya ya hewa kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.

Volodymir Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymir ZelenskyPicha: Jacob King/empics/picture alliance

Kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelenskyamesema anausifu "uamuzi mgumu lakini wenye nguvu" wa rais wa Marekani Joe Biden wa kusitisha azma yake ya kuchaguliwa tena na amemshukuru Rais huyo wa Marekani kwa kuchukua hatua za kijasiri katika kuiunga mkono nchi yake na jitihada zake za kuisadia Ukraine katika vita vya kutisha tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo.

Soma Pia: Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka 

Wengine ni Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ambaye amesema katika miaka ya utumishi wa Biden, upendo wa nchi yake umekuwa ndio ngao yake kuu.

Wizara ya Mambo ya Nje yaChina na naibu mkuu wa Baraza la Usalama la Urusi Dmitry Medvedev, wamesema kujiondoa kwa Joe Biden kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Marekani kuna madhara kwa sababu kumesababisha hali ya kutokuwa na uhakika duniani wakati ambapo viongozi wa Magharibi wanakabiliana na vita vya Ukraine, katika Ukanda Gaza, China yenye uthubutu, kujiamini zaidi nchi za Asia na kuongezeka kwa mrengo wa kulia barani Ulaya.

Soma Pia: Uchaguzi wa Marekani: Makamu wa rais Kamala Harris ni nani?

Masoko ya hisa barani Asia yaliporomoka siku Jumatatu kutokana na uamuzi wa Joe Biden wa kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais wa Marekani na hatua hiyo imezidisha hali ya sintofahamu.

Joe Biden na kamala Harris
Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia Makamu wa Rais wa Marekani Kamala HarrisPicha: William T. Wade Jr./Photography/Avalon/picture alliance

Rais Joe Bidenbaada ya kutangaza kujiondoa kwake kwenye kugombea urais wa Marekani mnamo siku ya Jumapili 21.07.2024 alimuidhinisha makamu wake Kamala Harris, kama mteule mpya wa Chama cha Democratic katika kinyang'anyiro cha urais ambapo atapambana na mgombea wa chama cha Republican rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Vyanzo: AFP/DPA/AP