1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Uchaguzi wa Marekani: Makamu wa Rais Kamala Harris ni nani?

22 Julai 2024

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ndiye wa kwanza kwenye orodha ya watakaochukua nafasi ya Joe Biden – katika Ikulu ya White House na katika mbio za urais za 2024 dhidi ya Donald Trump.

https://p.dw.com/p/4iZMy
Uchaguzi wa rais Marekani
Harris aligombea dhidi ya Biden katika uteuzi wa chama kabla ya kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguziPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Wakati Kamala Harris alikubali kuwa mgombea mwenza wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais na akaushika mkono wa Biden jukwaani Agosti 2020, mustakabali wa viongozi hao wawili ulionekana kuwa mzuri.

Biden alikuwa mbioni kumuondoa Donald Trump na kurejesha hisia ya hali ya kawaida nchini Marekani, kwa sehemu kubwa kutokana na uzoefu wake wa kisiasa wa muongo mmoja. Harris alikuwa kiongozi mwenye haiba, mwenye nguvu kwa ajili ya enzi mpya - mwanamke mweusi na mtoto wa wazazi wahamiaji - ambaye aliingia katika siasa baada ya kupambana kutokea chini na kuwa mwendesha mashtaka mkuu wa umma jimboni California.

Harris sasa huenda akaitwa kuinusuru tiketi ya urais ya Wademocrat na kukabiliana na Donald Trump katika uchaguzi wa Novemba. Lakini mwangaza wake umefifia wakati wa miaka yake minne katika Ikulu ya White House.

Hadithi ya Harris' ya Marekani

Uchaguzi wa rais Marekani
Harris ni mwanamke wa kwanza mweusi na mwenye asili ya Kihindi kuwa makamu wa rais wa Marekani.Picha: Courtesy of Kamala Harris/AFP

Kamala Harris alizaliwa katika familia ya wahamiaji mjini Oakland, California, mwaka wa 1964. Mamake Harris alikuwa mtafiti wa saratani ya matiti mzaliwa wa India Shyamala Gopalan, babake alikuwa profesa wa Uchumi Donald J. Harris kutoka Jamaica. Wazazi wake Harris wote walijihusisha na vuguvugu la haki za kiraia la miaka ya 1960.

Ndoa ya wazazi wake ilivunjika wakati Kamala alikuwa na umri wa miaka 7. Miaka mitano baadae, mama yake alipata kazi ya utafiti nchini Canada na familia hiyo ikahamia Montreal.

Harris alipata elimu ya sekondari nchini Canada. Kisha akarudi Marekani kusomea sayansi ya siasa na Uchumi mjini Washington DC, na kisha katika jimbo lake la California kusomea sheria mwaka wa 1986. Alihitimu kama mwanasheira mwaka wa 1990 na akaanza taaluma yake kama mwendesha mashitaka, kabla ya kupanda ngazi na kuwa mwanasheria mkuu wa California mwaka wa 2011. Alikuwa mwanamke wa kwanza, Mmarekani mweusi mwenye asili ya Kusini mwa Asia kushikilia wadhifa huo.

Harris mwendesha mashitaka California

Taaluma ya Harris ya mwendesha mashitaka ilikuwa mfuko wenye mambo mseto. Alijifanya kuwa “askari mkuu” wa California lakini akawakasirisha polisi kwa kukataa kutoa hukumu ya kifo hata katika kesi ambazo maafisa wa polisi waliuawa. Wakati huo huo, alikosolewa kwa kutofanya vya kutosha kupambana na ufisadi katika idara ya polisi.

Uchaguzi wa rais Marekani
Biden amempendekeza Kamala Harris kuchukua nafasi yake katika mbio za Ikulu ya White HousePicha: Ricky Fitchett/ZUMA Press Wire/picture alliance

Katika mwaka wa 2015, alitangaza kuwa anagombea Useneta na akapata uungaji mkono wa Joe Biden na rais wa wakati huo Barack Obama. Mwaka wa 2017, akawa mwanamke wa pili mweusi kuhudumu katika Baraza la Seneti. Katika mwaka wa 2019, alianzisha kampeni ya kugombea uteuzi wa Democratic katika uchaguzi wa rais huku Biden akiwa mmoja wa wapinzani wake. Harris hatimaye alijiondoa katika mbio za urais na akamuunga mkono Biden, ambaye baadae alimuomba kuwa makamu wake wa rais.

Mgogoro wa uhamiaji

Biden na Harris walipambana katika kampeni kali kwa pamoja na hatimaye wakakamuangusha Donald Trump na Makamu wa Rais Mike Pence. Waliapishwa Januari 20, 2021 wiki mbili tu baada ya umati wa watu kuvamia majengo ya bunge wakitaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe. Harris kwa mara nyingine akaweka historia – mwanamke wa kwanza, mtu wa kwanza mweusi na mtu wa kwanza mwenye asili ya Kihindi kuhudumu kama makamu wa rais wa Marekani.

Kazi hiyo ilimpa Harris mamlaka ya kuchukua serikali kama rais angefariki au asiweze kutekeleza majukumu yake. Lakini Harris amekabiliwa na changamoto kuimarisha haiba yake wakati wa muda wake katika Ikulu ya White House.

Katika mwaka wa 2021, Biden alimpa jukumu la kushughulikia uhamiaji kwa kupambana na “sababu kuu” za watu kuondoka Amerika Kusini. Zawadi hiyo iligeuka kuwa sumu. Licha ya juhudi za Harris na mikutano na viongozi wa Amerika Kusini, idadi ya wahamiaji wasio na vibali waliokuwa wakivuka mpaka iliendelea kuongezeka, na kufikia viwango vya juu zaidi mwaka jana. Warepublican walishambulia Harris kwa kushindwa kudhibiti idadi ya wahamiaji wanaovuka mpaka.