1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baerbock ahimiza Israel kujizuia dhidi ya Hezbollah

Iddi Ssessanga | Hawa Bihoga
26 Juni 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameionya Israel dhidi ya makosa mabaya yanayoweza kusababisha vita kamili kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon, akihimiza kujizuia.

https://p.dw.com/p/4hWhZ
Waziri wa Mambo ya Nje Ujerumani Annalena Baerbock akizungumza katika mkutano.
Waziri wa Mambo ya Nje Ujerumani Annalena Baerbock akizungumza katika mkutano.Picha: Thomas Koehler/AA/picture alliance

Baerbock ambaye amefanya ziara yake ya nane Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa vita vya Gaza, pia ametangaza msaada mwingine wa kiutu wa dola milioni 19 kwa ajili ya eneo hilo la Wapalestina. 

Akizungumza katika mkutano wa usalama mjini Tel Aviv Waziri Baerbock alisema wakati wa ziara mjini Beirut kuwa kwa kila roketi inayovuka msitari wa Bluu kati ya Lebanon na Israel, hatari inaongezeka kwamba makosa yanaweza kusababisha vita kali, na kutoa wito kwa pande zote kujizuwia.

Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani aliionya pia kama "rafiki" wa karibu wa Israel kwamba inaweza "kupoteza" katika vita vyake vinavyoendelea dhidi ya kundi la Hamas na kuongeza kwamba kuongezeka kwa hali ya hasira kwa raia wa Ukanda wa Gaza kunadhoofisha usalama wa Israel.

''Ni mara ngapi, katika miezi michache iliyopita, nimejiuliza: Ningefanya nini ikiwa watoto wangu wangekuwa bila mimi na mume wangu huko Gaza." Aliuliza hadhira katika mkutano huo ambao ni muhimu kwa utulivu hasa katika eneo la mashiriki ya kati.

Soma pia:Mivutano ya Israel-Hezbollah yaongeza hofu ya kutanuka vita vya Gaza

Aliongeza kwamba picha kutoka Gaza, zinasafiri kote ulimwenguni, zikizua hisia kali  katika ulimwengu wa Kiarabu, lakini pia nchini Marekani, barani Ulaya na kila mahali.

"Mshangao, huzuni, hasira. Na kama rafiki wa Israeli, nataka niwe mkweli: Hasira hii haiisaidii Israeli kukidhi mahitaji yake ya usalama, kinyume chake, inaisadia tu Hamas kuchochea ongezeko zaidi.''

Juhudi za upatanishi

Baerbock aliongeza kwamba kufanya juhudi kama zinazochukuliwa na wapatanishi wengine kama vile Marekani na Ufaransa ni muhimu zaidi kufanyika pia katika eneo la mpaka wa kaskazini wa Israel na Lebanon.

Jordan I Ukanda wa Gaza | Mkutano wa kujadili msaada wa kiutu Gaza
Mawaziri wa Mambo ya Nje wakiwa katika mkutano unaohusu kujadili kuongeza misaada ya kiutu Gaza inayokabiliwa na njaa iliofanyika Jordan Juni 11,2024Picha: Alaa Al-Sukhni/Pool/AFP

Katika ziara yake iliopita ya mwezi Januari Baerbock aliahidi kititia cha yuro milioni 15 katika kuliimarisha jeshi la Lebanan, ambalo kama zilivyo taasisi nyingine za kitaifa limekabiliwa na mzozo wa kifedha tangu uchumi wa nchi hiyo uliporomoka mwishoni mwa 2019.

Soma pia:Netanyahu asema hatokubali mpango unaokomesha vita Gaza

Wanadiplomasia kadhaa wa Mataifa ya Magharibi wamefanya ziara nchini Lebanon katika miezi ya hivi karibuni, wakitaka kupunguza mvutano wa mpakani, akiwemo mjumbe wa Marekani Amos Hochstein.

Mapigano yaendelea Ukanda wa Gaza

Wakati hayo yakiendelea ndani ya Ukanda wa Gaza vikosi vya Israel vimeendelea kushambulia maeneo kadhaa kote Gaza, ambapo wakaazi wameripoti mapigano makali ya usiku kucha hasa katika mji wa Rafah ambapo idadi kubwa ya Wapalestina wamejihifadhi.

Tawi la Hamas katika eneo hilo pamoja na washirika wao kundi la Islamic Jihad wamesema wapiganaji wake walijibu mashambulizi ya vikosi vya Israel.

Soma pia:Ripoti mpya inaonesha hatari kubwa ya njaa inaigubika Gaza

Nalo jeshi la Israel katika taarifa yake limearifu kwamba mimemuuä afisa mmoja wa Hamas ambae alikuwa akihusika na ulanguzi wa silaha kupitia mpaka kati ya mji wa kusini mwa Gaza Rafah na Misri.

Baerbock ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

Mashambulizi ya Israel ya kulipiza kisasi hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 37,658, na wengine maelfu wakijeruhiwa kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas, huku yakisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia.