1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu asema hatokubali mpango unaokomesha vita Gaza

24 Juni 2024

Ufanisi wa mpango wa Rais wa Marekani Joe Biden kumaliza vita vya Gaza umeingia mashakani, baada ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kusema atakuwa tayari kukubaliana tu na mpango ambao hautamaliza vita hivyo.

https://p.dw.com/p/4hQnA
Ukanda wa Gaza 2023 | Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu akizuru wanajeshi
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizuru vikosi vyake vinavyopigana Gaza.Picha: Avi Ohayon/GPO/ZUMA Press Wire/picture alliance

Katika mahojiano yaliyotangazwa Jumapili jioni kupitia kituo cha utangazaji cha Channel 14, kituo cha kihafidhina, kinachomuunga mkono Netanyahu, kiongozi huyo wa Israel alisema amejitayarisha kufanya makubaliano ya sehemu ambayo yatasaidia kurudisha baadhi ya mateka wapatao 120 wanaoendelea kushikiliwa katika Ukanda wa Gaza.

''Iwapo kutakuwa na makubaliano, yatakuwa makubaliano yanayofuata masharti yetu, na masharti yetu siyo kumaliza vita, kuondoka Gaza na kuiacha Hamas kama ilivyo. Ninakataa kuiacha Hmas kama ilivyo. Tunahitaji kuiondoa,'' alisema Netanyahu.

Soma pia: Netanyahu aishutumu Marekani kwa kuzuia msaada wa silaha

Netanyahu alisema awamu ya mapambano makali dhidi ya Hamas inakaribia kumalizika, na baada ya hapo watahamisha baadhi ya vikosi upande wa kaskazini, kwanza kwa sababu za kujilinda na pili kwa ajili ya kurudisha wakaazi waliohamishwa nyumbani.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anasema hatositisha vita Hamas ikiwa bado ina uwezo wa kijeshi la kiutawala Gaza.Picha: Menahem Kahana/AFP

Matamshi hayo hayakutofautiana pakubwa ya kile ambacho amekisema kabla kuhusu masharti ya makubaliano, lakini yamekuja wakati nyeti ambapo Israel na Hamas  zinaonekana kuzidi kutofautiana kuhusu pendekezo la karibuni zaidi la usitishaji vita, na yanaweza kuwakilisha kikwazo kingine kwa wapatanishi wanaojaribu kumaliza vita hivyo.

Matamshi hayo ya Netanyahu pia yamekwenda kinyume kabisaa na yale aliyoyatoa Rais Joe Biden wakati akiwasilisha pendekezo la mpango wa amani, ambalo alilitaja kuwa la Israel, na ambao baadhi ya Waisrael wanautaja kama mpango wa Netanyahu.

Matamshi yake yanaweza kuzorotesha zaidi uhusiano wa Israel na Marekani, mshirika wake mkuu, ambayo ilianzisha msukumo mkubwa wa kidiplomasia kwa pendekezo lake la karibuni zaidi la kusitisha mapigano.

Soma pia: Hamas yaitaka Marekani kuishinikiza Israel kusitisha vita Gaza

Mpango huo wa awamu tatu ungepelekea kuachiliwa kwa mateka waliosalia huku mamia ya Wapalestina waliofungwa nchini Israel wakiachiliwa pia. Lakini mabishano na kutoaminiana vinaendelea kati ya Israel na Hamas kuhusu jinsi mpango huo unavyotekelezwa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu afanya ziara Berlin

Hamas imesisitiza kuwa haitowaachilia mateka waliosalia hadi kuwepo na usitishaji wa kudumu wa mapigano na uondoaji kamili wa vikosi vya Israeli kutoka Gaza. Wakati Biden alipotangaza pendekezo la hivi karibuni mwezi uliopita, alisema lilijumuisha masuala yote mawili.

Lakini Netanyahu amesema Israel bado imedhamiria kuvunja uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas, na kuhakikisha kuwa haiwezi tena kufanya shambulio la mtindo wa Oktoba 7.

Kuondolewa kamili kwa vikosi vya Israeli kutoka Gaza, ambapo uongozi wa juu wa Hamas na sehemu kubwa ya vikosi vyake bado viko imara, kutaliacha kundi hilo likiwa na udhibiti wa eneo hilo na kuweza kupata tena silaha. Katika mahojiano hayo, Netanyahu alisema kuwa awamu ya sasa ya mapigano inakamilika, lakini hiyo haimaanishi kuwa vita vimekwisha.

Israel yamuuwa afisa wa juu wa afya Gaza

Kutokan Gaza kwenyewe, wizara ya afya ya ukanda huo imesema shambulio la Israel lililolenga kliniki limemua mkurugenzi wa idara ya- dharura na huduma za kusafirisha wagonjwa Hani al-Jaafarawi, huku jeshi la Israel likisema shambulio lake limemlenga Mohammad Salah, kamanda wa juu anaehusika na utengenezaji wa silaha za Hamas.

Ukanda wa Gaza| msaada kwa watu waliojeruhiwa
Mashambulizi ya Israel yameuwa watumishi 500 wa afya Gaza, na zaidi ya 300 wamekamatwa.Picha: Ali Hamad/APA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Soma pia: Qatar yataka misimamo ya wazi kuhusu mpango wa Gaza

"Salah alikuwa sehemu ya mradi wa kutengeneza silaha za kimkakati kwa shirika la kigaidi la Hamas, na aliongoza vikosi vya kigaidi vya Hamas ambavyo vilifanya kazi ya kutengeneza silaha," lilisema jeshi la Israel katika taarifa yake.

Wizara ya afya imesema mauaji ya al-Jaafarawi yamefikisha jumla ya wafanyakazi 500 wa afya waliouawa katika mashambulizi ya Israel tangu Oktoba 7, na wengine wasiopungua 300 wamekamatwa.

Borrell, Baerbock waeleza hofu mzozo kati ya Israel na Hezbollah

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameonya leo juu ya mzozo wa Gaza kusambaa nchini Lebanon, kutokana na mvutano unaozidi kwenye mpaka wa nchi hiyo na Israel, ambayo vikosi vyake vimekuwa vikishambuliana na wapiganaji wa kundi la Hezbollah kwa muda sasa.

Borrell alisema hali kwenye mpaka wa Israel na Lebanon inazidi kuwa mbaya.

Baerbock ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

Israel inatumia shinikizo la kijeshi na kidiplomasia kwa Hezbollah kwa lengo la kuwafanya wanachama wake warudi nyuma ya Mto Litani, umbali wa kilomita 30 kutoka mpakani - kama ilivyoainishwa katika azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa 2006.

Soma pia: Mapigano yachacha Gaza huku hofu ikizidi juu ya kusambaa kwa vita

Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant ameonya kwamba operesheni kubwa zaidi ya kijeshi huenda ikafuatwa ikibidi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alisema "kuongezeka zaidi kutakuwa janga kwa watu wote" katika Mashariki ya Kati.

Baerbock alizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg. Alirudia wito wake wa kusitishwa kwa mapigano Gaza kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Rais Joe Biden wa Marekani.

Borell alisema Hamas na Israel hazionyeshi nia ya kisiasa ya kuunga mkono mpango wa kusitisha mapigano wa Biden. Pia alisema msaada muhimu zaidi unahitajika kuingia kwenye ukanda huo.

Vitisho vya hivi karibuni vya vuguvugu la Hezbollah dhidi ya kisiwa cha Umoja wa Ulaya cha Cyprus kuhusu ushirikiano na Israel pia vinajadiliwa.

Chanzo: Mashirika