1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani azuru Mashariki ya Kati

Daniel Gakuba
8 Juni 2019

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amewasili Iraq, katika ziara itakayomfikisha katika nchi kadhaa za Mashariki ya Kati. Lengo la ziara hiyo ni kuhimiza stahamala wakati mivutano ikishamiri katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/3K3yM
Maas beginnt Krisen-Mission mit Truppenbesuch in Jordanien
Picha: picture-alliance/dpa/M. Fischer

Ziara ya waziri Heiko Maas nchini Iraq ilikuwa haikutangazwa katika ratiba ya safari yake kwa sababu za kiusalama. Mjini Baghdad anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Adel Abdel Mahdi, pamoja na Rais  Batham Salih.

Akizungumza baada ya kuwasili Iraq, Maas  amesema ''kuna kitisho cha dhahiri cha hatari isiyotabirika, inayoweza kutokana na kukadiria vibaya, uchokozi na kuelewa visivyo azma ya upande mwingine katika eneo hilo lenye mivutano mikali''.

Soma zaidi:  Marekani haipingi mfumo wa biashara wa Ulaya kuisaidia Iran

Akitoka Iraq Jumapili, waziri huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuendelea na ziara yake kwa kuzitembelea  Umoja wa Falma za Kiarabu na Jordan, kabla ya kufika Iran ambako ni kilele cha ziara hiyo. Katika mazungumzo na viongozi wa Iran, Maas atapigia debe kuendelezwa kwa mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, uliosiniwa mwaka 2015 baina ya nchi hiyo na mataifa yenye nguvu duniani.

Ulaya kujitwisha jukumu la upatanishi

Heiko Maas ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu mvutano kati ya Marekani na Iran ambao amesema umefika katika kiwango cha kutisha, akisema ni jukumu la nchi za Ulaya kuongoza njia katika matika mazungumzo ya kuutanzua mzozo huo.

Maas beginnt Krisen-Mission mit Truppenbesuch in Jordanien
Waziri Heiko Maas anasema Ulaya inayo kila sababu ya kutaka kuepusha mizozo Mashariki ya KatiPicha: picture-alliance/dpa/M. Fischer

''Kupanuka kwa uhasama kunatulazimu sisi kama majirani wa nchi za Ulaya, kuingilia kati kuhimiza ustahimilivu na kuishi kwa amani.'' Amesema waziri Maas na kuongeza kuwa ulazima wa kusaka suluhisho unaongezeka pale tofauti zinapooneka kubwa kiasi cha kukosa suluhu, au pale mivutano inapofikia kilele.

Mwaka jana, Marekani ilichukuwa uamuzi wa peke yake wa kujiondoa katika mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambao ulilenga kuizuia nchi hiyo kuunda silaha za atomiki, na imeanza kutekeleza vikwazo vikali dhidi ya sekta za mafuta na za kibenki za Iran, ambavyo vimeulemaza uchumi wa taifa hilo la Kiislamu.

Uamuzi wa Marekani waziacha nchi za Ulaya mahali panapoteleza

Hatua hiyo ya Marekani imeziacha katika hali ngumu nchi za Ulaya ambazo zinataka kuudumisha mkataba huo.

Bayern - Bundesaußenminister Maas mit Mohammed Dschawad Sarif
Nchi za Ulaya zinataka kudumishwa kwa Makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa IranPicha: picture-alliance/dpa/T. Hase

Mwezi uliopita, rais wa Iran Hassan Rouhani alizipa nchi hizo za Ulaya muda wa siku 60 kuiondolea vikwazo nchi yake, la sivyo itaanza kurutubisha tena madini ya urani.

Maas amesema Ulaya inaamini kwa dhati kwamba kila juhudi inahitajika kuhakikisha kuendelea kuwepo kwa mkataba huo uliosainiwa mjini Vienna.

Wakati mvutano ukishamiri kwenye Ghuba ya Uajemi, Marekani imeishutumu Iran kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli nne za kubeba mafuta, zilizokuwa zimetia nanga kwenye bandari ya Fujirah katika Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi uliopita. Iran imekanusha shutuma hizo, ambazo imesema zinalenga kuzidisha uhasama katika ukanda huo tete.

Soma zaidi: Marekani yasema inataka kuizuia Iran, si vitai:  

Kuna hofu kwamba mvutano huo baina ya Marekani na Iran unaweza kuenea hadi nchini Iraq, ambako yapo makundi wa wanamgambo wa Kishia wanaosaidiwa na Iran. Iraq inazo pia kambi za Marekani zenye maelfu ya wanajeshi wanaoisaidia Iraq katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

dpae, ape