1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani haipingi mfumo wa biashara wa Ulaya kuisaidia Iran

Sekione Kitojo
31 Mei 2019

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema kwamba nchi yake haitaziba njia dhidi ya mfumo wa mataifa ya Ulaya  unaotayarishwa kuyakinga makampuni yanayofanya biashara na Iran dhidi ya vikwazo vya Marekani.

https://p.dw.com/p/3JZXs
Berlin Bundesaußenminister Heiko Maas trifft US Außenminister Pompeo
Picha: Imago Images/photothek

Iwapo  tu  lengo  ni  kutoa  huduma  ya  kiutu na  bidhaa  nyingine zilizoruhusiwa hilo  halina  taabu. Pompeo  ameyasema  hayo  mbele ya waandishi habari  baada  ya  kukutana  na  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa Ujerumani  Heiko Maas. 

Berlin US Außenminister Pompeo bei Maas
Mike Pompeo (kushoto) akiwa pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas(kulia)Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Pompeo  akifanya  ziara  yake  ya  kwanza  nchini  Ujerumani  akiwa waziri  wa  mambo  ya  kigeni , amesema  Marekani  haizuwii utayarishaji  wa  mfumo  unaofahamika  kama  INSTEX, iwapo  tu utashughulika  na  biashara  ya  bidhaa  ambazo  hazimo  katika orodha  iliyowekewa  vikwazo, kama  ambavyo mataifa  ya  Ulaya yanavyofikiria  kuwa  itakuwa  hivyo.

"tumekuwa  wawazi kabisa  juu  ya  biashara  na  Iran, kuna  bidhaa ambazo zimewekewa  vikwazo na  kuna  bidhaa ambazo hazikuwekewa   vikwazo," Pompeo  amewaambia  waandishi  habari baada  ya  mkutano  na  waziri  mwenzanke  wa  Ujerumani  Heiko Maas katika  jengo  la  serikali  mjini  Berlin.

"Wakati  tukifikiri  kuhusu INSTEX , iwapo mfumo  huu  unalenga katika  kutoa  huduma  ya  usafirishaji  wa  bidhaa  ambazo zinaruhusiwa  kusafirishwa, hakuna  taabu," alisema. Pompeo alikutana  kwanza na  kansela  Angela  Merkel  wa  Ujerumani  kabla ya  kukutana  na  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  Heiko Maas.

Deutschland Berlin | US Außenminister Mike Pompeo auf Staatsbesuch mi Angela Merkel
Mike Pompeo (Kushoto) akiwa pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel(kulia)Picha: Reuters/F. Bensch

Jinsi ya  kuizuwia Iran

Pompeo  aliwaambia  waandishi  habari  kabla  ya  kuanza  ziara yake  nchini  Ujerumani  kwamba  mazungumzo  yatatuwama  katika makubaliano  ya  kinyuklia  na  Iran, masuala  yanayolihusu shirika la  mawasiliano  la  China  Huawei  pamoja  na  matumizi  ya  kijeshi ya  Ujerumani, yote  yakiwa  masuala  muhimu  katika  uhusiano  kati ya  washirika  hao  wanaopakana  na  bahari  ya  Atlantiki.

Kabla ya  mazungumzo   na  Mike Pompeo leo, kansela  wa Ujerumani  Angela  Merkel  alisema:

"Tutajadili matatizo  mbali  mbali, dunia imo katika  hali  ya  wasi wasi mkubwa, hususan  suala  la  Iran na  vipi tunaweza  kuzuwia Iran kujipatia  silaha  za  kinyuklia, vipi tutaweza  kuzuwia  hatua za kimabavu na uchokozi za  Iran, tutazungumzia  kuhusu Afghanistan, ambako wote tuna vikosi vya  jeshi, tutazungumzia  pia  juu  ya  hali nchini  Syria  na  bila  shaka  hali tete  nchini  Libya."

Deutschland Bundeskanzlerin Merkel und der US Außenminister Pompeo
wakizungumza na waandishi habari waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo (kushoto) na kansela Angela Merkel (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani  Heiko Maas amesema  licha  ya  kuwa  Marekani  haishiriki  tena  katika makubaliano  na  Iran, yanayofahamika  kama  mpango wa  pamoja wa  kuchukua  hatua ama  JCPOA, lengo  lake  ni  hilo  hilo. Pompeo yuko  katika  ziara  ya  mataifa  manne ya Ulaya  ambapo  pia atafika nchini  Uswisi, na  Uholanzi, kabla  ya  kuungana  na  rais Trump katika  ziara  yake  nchini  Uingereza.