1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina 2,220 wameuawa kwa mashambulizi ya Israel

Angela Mdungu
15 Oktoba 2023

Mashambulizi ya Israeli katika ukanda wa Gaza yameshawauwa zaidi ya watu 2,200 tangu Hamas ilipovamia Israel wiki moja iliyopita. Wizara ya afya ya Gaza imesema watoto 724 na wanawake 458 ni miongoni mwa wahanga.

https://p.dw.com/p/4XXMo
Gazastreifen Khan Younis Rettungsarbeiten nach Luftangriff
Picha: Belal Khaled/Anadolu/picture alliance

Takwimu hizo zimetolewa baada ya taarifa ya awali iliyosema kuwa watu wasiopungua 324 wameuwawa katika saa 24 zilizopita kutokana na mashambulizi yanayoendelea.

Taarifa hiyo imetolewa wakati jeshi la Israel likisisitiza tena leo Jumamosi 14.10.2023 kuwa, wakaazi wa Gaza ni lazima waondoke katika eneo la kaskazini la mji huo kabla ya kuanza kwa mashambulizi.

Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa jeshi la Israel, IDF, Richard Hecht ambaye ameongeza kuwa, kuna muda salama wa kuondoka kwenye mji huo kati ya saa nne asubuhi na saa kumi jioni kuelekea katika Pwani ya Gaza, ambapo kuna umbali wa takribani kilometa 40.

Soma zaidi: Maelfu wakimbilia kusini mwa Gaza kukwepa jeshi la Israel

Hecht amesema wanajua itachukua muda kwa wakaazi hao kuhama, lakini wamewashauri wasikawie kuondoka. Njia mbili salama zimetengwa  ili kuwaruhusu zaidi ya wakaazi milioni 1.1 wa Gaza kuondoka kuelekea kusini mwa ukanda huo.

Wakaazi wa Gaza wakizima moto baada ya mashambulizi ya anga kutoka Israel
Wakaazi wa Gaza wakizima moto baada ya mashambulizi ya anga kutoka IsraelPicha: Yasser Qudih/AFP/Getty Images

Maelfu ya wakaazi hao wameonekana wakiwa wamejaa kwenye mabasi, magari na mikokoteni ya Punda wakilikimbia eneo la kaskazini.

Israeli inatarajiwa kuanzisha operesheni ya ardhini dhidi ya kundi la Hamas lililoshambulia kusini mwa Israel Oktoba 7. Marekani, Umoja wa Ulaya na Ujerumani ikiwemo, pamoja na nchi nyingine kadhaa, huichukulia Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Juhudi za kufungua mpaka kivuko cha Rafah zinaendelea

Wakati joto la kutakiwa kuondoka Gaza likizidi kuongezeka, Marekani imesema imekuwa ikifanya kazi kwa pamoja na Israel, Misri na Qatar ili kufungua mpaka katika kivuko cha Rafah kutoka Gaza kuelekea Misri. 

Marekani imesema imefanya mazungumzo ya kuruhusu kufunguliwa kwa muda kwa mpaka wa Rafah kutoka Gaza ili kuwaruhusu raia wa Marekani kuondoka kwenye ukanda huo.

Kulingana na magazeti ya New York Times na Washington Post yaliyomnukuu afisa wa ngazi ya juu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, serikali za Israel na Misri zilikubaliana kuwaruhusu raia wake kuondoka Gaza leo Jumamosi kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Vikosi vya usalama vya Palestina vikilinda doria Rafa
Vikosi vya usalama vya Palestinanvikilinda doria RafaPicha: Ashraf Amra/Zuma/IMAGO

Hata hivyo wafuatiliaji katika eneo hilo la mpaka wamesema hawajaona dalili za kufunguliwa kwa mpaka huo ndani ya wakati uliopangwa.

Israel na madai ya kuwauwa baadhi ya makamanda wa Hamas

Wakati juhudi hizo za kufungua mpaka huo zikiendelea, Jeshi la Israel limesema limefanikiwa kumuuwa Ali Qadi, Kamanda wa Hamas aliyeongoza vikosi vilivyowauwa raia katika shambulizi la ghafla la wiki iliyopita kusini mwa Israel.

Taarifa ya jeshi hilo imesema ndege yake ya Kijeshi ilimuuwa Qadi wa kikosi cha Nukhba cha Hamas bila kutaja mahali na muda aliouwawa.

Mmoja wa maafisa wa kundi hilo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema kuwa kundi hilo halina chochote cha kusema kuhusu madai ya kuuwawa kwa kamanda huyo ingawa alithibitisha kuwa Qadi alikuwa kamanda wa kikosi maalumu cha Hamas.

Taarifa zote za Afisa wa Palestina na ya Jeshi la Israel zilisema kuwa kamanda huyo alikuwa mmoja wa zaidi ya wafungwa 1,000 wa Palestina walioachiliwa huru na Israel mwaka 2011 baada ya Palestina kumuachilia mwanajeshi wa Israel Gilad Shali aliyekamatwa na Hamas mwaka 2006. 

Qadi alikamatwa na Israel mwaka 2005 kwa tuhuma za kumteka nyara na kumuuwa mwanamume wa Kiisraeli aliyetambuliwa kama wakala wa shirika la usalama wa ndani wa Israel, Shin Bet.

Soma zaidi: Iran, Saudi Arabia zasaka suluhu Gaza

Kando ya Qadi, Israel imesema pia kupitia mashambulizi yake imewauwa Ali al Kadhi ma Merad Abu wanaoshukiwa kuhusika na shambulio la Hamas lililofanywa kusini mwa Israel Oktoba 7. 

Khadi alikuwa mfungwa aliyeachiliwa na Israel katika makubaliano ya kubadilishana wafungwa mwaka 2005 ambapo alirejea katika ukanda wa Gaza.

Aliwahi kufungwa kwa makosa ya utekaji nyara na mauaji ya raia wa Israel. Jeshi la Israel limetoa taarifa hiyo baada ya hapo awali kutangaza tena kuwa limemuuwa mtu mwingine anayetuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya oktoba 7, Merad Abu Merad

Ndege za misaada kwa ajili ya Wapalestina zawasili Misri

Wakati huohuo, Afisa mmoja wa shirika la hilali nyekundu amesema kuwa ndege zilizobeba misaada zimewasili katika rasi ya Sinai ambako misaada imekuwa ikizuiwa mpaka itakapopatikana njia salama ya kuifikisha karibu na ukanda wa Gaza.

Misri imesema, sehemu ya upande wake wa mpaka wa Rafah unaoiunganisha Sinai na ukanda wa Gaza inasalia kuwa wazi ingawa usafiri umezuiwa kwa siku kadhaa kutokana na mashambulizi ya Israel yanayoelekezwa kwenye upande wa mpakani wa Palestina.

Katika taarifa nyingine inayohusiana na mzozo huo, Saudi Arabia imesimamisha mazungumzo yake na Marekani yaliyolenga kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel kutokana na mashambulizi ya anga ya Israeli katika ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia.

Majeshi ya Israel yakielekea katika mpaka wa Gaza karibu na mji wa Sderot
Majeshi ya Israel yakielekea katika mpaka wa Gaza karibu na mji wa SderotPicha: Amir Levy/Getty Images

Taarifa hizo zimetolea baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken kuwasili Saudia, kama sehemu ya ziara ya kikanda wakati vita kati ya Israel na kundi la Hamas vikipamba moto. Mwezi uliopita mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman alithibitisha kupigwa kwa hatua kuelekea kurejesha mahusiano kati ya taifa lake na Israel.

Vyanzo: AFP/DPA/