1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Ajenda ya mahusiano kati ya Israel na mataifa ya kiarabu

12 Oktoba 2023

Baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel, mwelekeo wa kurekebisha uhusiano kati ya Israel na Saudi Arabia umebadilika na kugeuka kuwa mshikamano wa mataifa ya kiarabu kwa Wapalestina.

https://p.dw.com/p/4XRpu
Israel VAE | Netanjahu Flughafen Ben-Gurion | Ankunft Flieger
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) alipohudhuria sherehe za kuanzishwa safari za shirika la ndege la flydubai nchini Israel (26.11.2020).Picha: Emil Salman/AP/picture alliance

Wito umekuwa ukiongezeka wa kufikiwa suluhu ya kuwa na mataifa mawili. Swali ni Je, Hamas imeibua upya ajenda ya kurekebisha mahusiano kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu?

Mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na wanamgambo wa Kiislamu wa Hamas dhidi ya Israel tayari yamesababisha madhara makubwa ambayo yamevuka hadi mipaka ya Israel na Gaza  na kuyaweka rehani matumaini kadhaa.

Ni wiki mbili tangu mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuthibitisha kuwa nchi zao zinakaribia kufikia makubaliano ya kurejesha rasmi mahusiano yao, hatua ambayo ingekua chanya kwa ukanda huo. Lakini kwa sasa hilo linaonekana kuwa kama ndoto.

Soma pia: Kwa nini mataifa ya Kiarabu yanakataa mahusiano na Israel

Aidha, msimamo wa bin Salman wa kutotilia maanani suluhisho la upatikanaji wa serikali mbili ambalo lingewawezesha Wapalestina kuwa na nchi huru huku Jerusalem Mashariki ikiwa kama mji mkuu, nalo limesahaulika.

Mohammed bin Salman Saudi Arabien
Mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: Leon Neal/empics/picture alliance

Mwishoni mwa mwezi Septemba, Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani Fox News, Mwanamfalme huyo wa Saudia hakutaja suluhisho hilo la serikali mbili, bali alitaja tu kwamba mkataba huo mpya na Israel "utawapa Wapalestina mahitaji yao na kuwahakikishia maisha bora."

kufufuliwa upya kwa suluhisho la serikali mbili

Kufuatia kuzuka kwa mapambano siku ya Jumamosi, Saudi Arabia imerejelea msimamo wake hadharani na kutetea suluhisho la serikali mbili na kujinadi waziwazi kama mshirika thabiti wa watu wa Wapalestina.

Soma pia: Iran yapinga mahusiano kati ya Israel na mataifa ya kiarabu

Wakati huo huo, nchi nyingine nyingi zimetangaza kuiunga mkono Israel na haki yake ya kujilinda. Kufufuliwa kwa suluhisho hilo la serikali mbili ni ushindi mkubwa kwa kundi la Hamas linaloungwa mkono na Iran, ambalo limetajwa kuwa kundi la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa mengine.

Richard LeBaron, Afisa mwandamizi katika Baraza la utafiti la Atlantiki lenye makao yake nchini Marekani, amesema vitendo vya Hamas vinatoa ukumbusho uliyo wazi kwa Saudia kwamba suala la Palestina lisichukuliwe kama mada rahisi tu katika mazungumzo yao huku LeBaron akiongeza kuwa mashambulizi hayo yatabadili simulizi au mwelekeo wa kurejesha mahusiano kati ya Saudi Arabia na Israel.

Uhusiano wa Israel na Saudia uko hatarini

Kombobild Netanjahu, Biden, Bin Salman
Mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman(kulia), Rais wa Marekani Joe Biden (katikati) na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto).Picha: Abir Sultan/EPA Pool/AP/Susan Walsh/Bandar Aljaloud/Royal Court of Saudi Arabia/picture alliance

Jonathan Panikoff, mkurugenzi wa Mpango wa Usalama wa Mashariki ya Kati wa Baraza la Atlantiki la Scowcroft, ameiambia DW kwamba katika siku za usoni, hakuna matarajio kwamba kutakuwa na maendeleo yoyote yatakayofikiwa katika mpango wa kurejesha mahusiano kati ya Saudia na Israel. Kwa maoni yake, masuala ya siasa na biashara ambayo yangehitajika, hayatowezekana tena ikiwa operesheni ya Israel itasababisha vifo na uharibifu mkubwa huko Gaza.

Soma pia: Waziri mkuu wa Israel ziarani Falme za Kiarabu

Siku ya Jumatatu (09.10.2023), Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alitoa amri ya kuizingira kabisa Gaza na kusema hakutakuwa na umeme, chakula au mafuta vitakavyowasilishwa huko Gaza.

Hugh Lovatt, mtafiti katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni, ameiambia DW kuwa anaamini kwamba maoni ya umma ya wakazi wa mataifa ya kiarabu, ambayo kwa kiasi kikubwa yamejawa na chuki dhidi ya Israel, yatazidisha chuki hiyo kutokana na hatua za Israel.

Soma pia: Saudia yaunga mkono juhudi za Marekani kwenye Mashariki ya Kati

Kituo cha habari kinachojikita na masuala ya kiuchumi "Bloomberg" kimeripoti kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao ulitia saini makubaliano ya kurekebisha mahusiano na Israel mwaka 2020, imetoa rambirambi kwa raia wa Israel waliouliwa na kutoa wito wa kuachana na mapigano lakini hawakulaani moja kwa moja vitendo vya kundi la Hamas.

USA | Protest vor dem Weißen Haus |  Jamal Khashoggi
Waandamanaji mjini Washington Marekani wakilaani mauaji ya Jamal Kashoggi na kutaka kuwepo haki.(19.10.2018)Picha: JIM WATSON/AFP/Getty Images

Si pekee shinikizo la Waarabu ambalo litatoa muelekeo katika maamuzi ya Saudi Arabia ikiwa itaendelea na makubaliano ya kurekebisha mahusiano na Israel.  Nchi Marekani na Iran zinalo jukumu kubwa.

Licha ya maridhiano ya mwaka huu kati ya Saudi Arabia na hasimu wake wa zamani  Iran, nchi hizo mbili bado zina mvutano linapokuja suala la washirika wao. Iran inaunga mkono Hamas inayotawala Gaza huku Saudi Arabia ikiwa mshirika wa Marekani.

Hata hivyo, Saudia ilikuwa na matumaini kwamba kurejesha uhusiano na Israel kungeisaidia pia kurekebisha uhusiano na Marekani kama ilivyokuwa kabla ya mauaji ya mkosoaji wa Saudia Jamal Khashoggi mnamo mwaka 2018.