1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel yalaaniwa

9 Oktoba 2023

Nchi nyingi wanachama wa Baraza la Usalama la UN zimelaani mashambulizi ya Hamas ya Jumamosi dhidi ya Israel, lakini Marekani na Israel zimekosoa kukosekana kwa kauli moja kutoka kikao cha dharura cha baraza hilo

https://p.dw.com/p/4XH4I
Mashambulizi ya anga yateketeza majengo katika Jiji la Gaza, Israeli mnamo Oktoba 8, 2023. Israel yatangaza vita dhidi ya kundi la Hamas
Mashambulizi ya anga yateketeza majengo katika Jiji la Gaza, Israeli mnamo Oktoba 8, 2023Picha: Mahmud Hams/AFP

Waisraeli zaidi ya 700 waliuawa katika mashambulizi hayo ya Hamas, wakiwamo zaidi ya 260 waliouawa katika tamasha la muziki. Wapalestina wasiopungua 400 pia wamepoteza maisha katika hujuma za Israel za kulipiza kisasi katika Ukanda wa Gaza.

Soma pia:Baada ya shambulio la Hamas, Netanyahu asema Israel iko vitani

Wanadiplomasia wamearifu katika kikao cha Baraza la Usalama, baadhi ya mataifa yakiongozwa na Urusi yalitaka mkutano huo uangazie masuala mapana zaidi badala ya kujikita juu ya Hamas.

Mataifa kadhaa yatangaza kusimama na Israel

Wakati huo huo, ziara ya ulinzi ya Marekani imesema inapeleka manowari yake ya kubebea ndege za kivita mashariki mwa bahari ya Mediterania, huku waziri wa ulinzi wa Marekani Llyod Austin akithibitisha kuwa nchi yake itaipatia Israel msaada zaidi wa silaha, na kuimarisha uwepo wa kijeshi wa Marekani katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Soma pia: Watu wasiopungua 40 wameuawa Israel katika mashambulizi ya Hamas

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akihudhuria kikao cha kila wiki cha mawaziri katika ofisi yake mjini Jerusalem mnamo Septemba 27, 2023
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Abir Sultan/Pool via REUTERS

Hali kadhalika Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amezungumza kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kumhakikishia kuwa Ujerumani inasimama bega kwa bega na Israel.

Mashirika makubwa ya ndege yafuta safari kuelekea Tel Aviv

Huku hayo yakijiri, mashirika makubwa ya ndege yamefuta safari zao kuelekea katika mji mkuu wa Israel, Tel Aviv wikendi hii iliyomalizika, kufuatia shambulio la Hamas dhidi ya Israel. American Airlines, Air France, Lufthansa, Emirates na Ryanair ni miongoni mwa mashirika hayo yaliyositisha safari katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion.

Soma pia:Israel yaufungua tena mpaka wake na Gaza

Hata hivyo, mamlaka za viwanja vya ndege  hazijasimamisha huduma za kibiashara na uwanja wa pili wa kimataifa nchini Israel wa Eilat ambao ni kituo cha watalii kwenye Bahari ya Sham. Israel imetangaza vita rasmi dhidi ya kundi la Hamas, ambapo waziri mkuu Benjamin Netanyahu ameapa kufika katika kila kona linakopatikana kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina.