1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo : jopo la wataalamu laamini ungwaji mkono kwa M23

Kiswahili24 Juni 2022

Jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limezishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 mashariki mwa Kongo. Madai ambayo Rwanda inayatupilia mbali.

https://p.dw.com/p/4DDU0
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wasema waasi wa M23 waungwa mkono na Rwanda na Uganda
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wasema waasi wa M23 waungwa mkono na Rwanda na UgandaPicha: Joseph Kay/AP Photo/picture alliance

Katika ripoti hiyo yenye kurasa 300, ambayo DW imepata nakala yake, Jopo la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu DRC linasema hali ya usalama na kibinadamu imezorota katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa waasi wa M23 walitumia Rwanda na Uganda kama msingi wa kujipanga upya. M23 inaishutumu serikali ya Kongo kwa kutowajumuisha kikamilifu wapiganaji wake katika jeshi na serikali kama ilivyoahidiwa katika mkataba wa 2009.

Jason Stearns,mtafiti kuhusu Kongo kwenye Chuo Kikuu cha NewYork amesema bila shaka Rwanda imewaunga mkono waasi wa M23.

''Tunapokea shuhuda zaidi na zaidi kutoka kwa watu walioko kwenye eneo la tukio na ambao wameona wanajeshi wakivuka mpaka. Tuna wenzetu ambao wamezungumza na wapiganaji wa M23 waliotoroka ambao wanashuhudia uwepo wa msaada wa Rwanda. Pia kuna wapiganaji wa M23 ambao tunawafahamu na wanaotupa ushuhuda wa aina hii.'',alisema Stearns.

Rwanda imekanusha mara kwa mara tuhuma hizo. Badala yake, taifa hilo linailaumu Kongo kwa kushirikiana na kundi la FDLR.
soma pia →Amnesty: Raia lazima walindwe Kongo

M23 waliajiri wapiganaji Uganda

Zaidi ya raia 60.000 wameyahama makazi yao
Zaidi ya raia 60.000 wameyahama makazi yaoPicha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa kuanzia Novemba 2021, waasi wa M23 walianza kuajiri wapiganaji katika kambi ya wakimbizi ya Bihanga, iliyoko kilomita 300 (maili 186) kusini magharibi mwa mji mkuu wa Uganda Kampala. Suala jingine pia lililoshughulikiwa katika ripoti hiyo ni upatikanaji wa vifaa vya kijeshi vilivyopitishwa kama "zana za kilimo."

Wiki hii, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliitisha mkutano wa ngazi ya juu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Mbali na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, wakuu wote wa nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiwemo; Kenya, Uganda, Rwanda, DRC, Burundi, Tanzania, na Sudan Kusini zilikuwepo.

Soma pia→Maelfu ya wakimbizi watoroka vita Kongo

Mapigano mapya kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo yamesababisha takriban watu 60,000 kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. Na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, imesema hii leo kuwa watoto zaidi ya mia nane wamepoteza mawasiliano na  wazazi wao kufuatia mapigano baina ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo.