1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Jeshi laanza rasmi jukumu la kuiongoza kwa muda Bangladesh

Angela Mdungu
6 Agosti 2024

Jeshi la Bangladesh limechukuwa rasmi udhibiti wa nchi Jumanne, baada ya maandamano makubwa ya umma kumlazimisha mtawala wa muda mrefu wa taifa hilo kujiuzulu na kukimbilia uhamishoni

https://p.dw.com/p/4j9dF
Dhaka, Bangladesh
Raia wakipongezana na wanajeshi mjini Dhaka baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzuluPicha: Mohammad Ponir Hossain/REUTERS

Rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin tayari amelivunja bunge katika utekelezaji wa hatua ambayo ni moja ya matakwa muhimu ya wanafunzi walioandamana. Taarifa ya kuvunjwa kwa bunge hilo imetolewa na katibu wa habari wa Rais Shiplu Zaman.

Mkuu wa jeshi Jenerali Waker-Uz-Zaman anatazamiwa kukutana na viongozi wa maandamano ya wanafunzi wakati taifa hilo likisubiri kuundwa kwa serikali mpya. Viongozi wa wanafunzi wamempendekeza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Muhammad Yunus kuongoza serikali ya mpito.

Soma zaidi: Nguvu ya vijana yaanguasha utawala wa miaka 15 Bangladesh

Pendekezo la mratibu muhimu wa maandamano yaliyofanywa na wanafunzi Nahid Islam kuwa Muhammad Yunus aongoze serikali ya mpito  limetolewa siku moja baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu.

Sheikh Hasina, Bangladesh
Mtawala wa Bangladesh Sheikh Hasina aliyekimbilia ubamishoni baada ya maandamanoPicha: Peerapon Boonyakiat/SOPA Images/IMAGO

Kauli hiyo imetolewa baada ya Mkuu wa jeshi la Bangladesh Waker-Uz-Zaman, kutoa hotuba kwa njia ya Televisheni na kutangaza kuwa jeshi hilo litaunda serikali ya mpito na kutaka maandamano yasitishwe.

Hali ya utulivu yarejea Dhaka

Mitaa katika mji mkuu Dhaka imeonekana ikiwa katika hali ya utulivu  Jumanne huku huduma za usafiri na biashara zikirejea katika hali ya kawaida. Licha ya hali hiyo, ofisi za serikali nchini humo zimeendelea kufungwa baada ya vurugu zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 300. 

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari, Waziri Mkuu Sheikh Hasina aliyekimbilia India, aliwasili katika uwanja wa ndege wa jeshi wa Hindon, ulio kilometa 30 kutoka Delhi jana Jumatatu.

Hayo yakijiri, Waziri wa mambo ya kigeni wa India Subrahmanyam Jaishankar ametoa hotuba katika mkutano wa faragha wa vyama vyote vya siasa ndani ya bunge mjini New Delhi ili kujadili mgogoro wa taifa jirani la Bangladesh. Waziri wa mambo ya ndani Amit Shah, na wa ulinzi Rajnath Singh sambamba na kiongozi wa upinzani Rahul Gandhi ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa wanaoshiriki kwenye mkutano huo.

Sheikh Hasina, Bangladesh
Mtawala wa Bangladesh Sheikh Hasina aliyekimbilia ubamishoni baada ya maandamanoPicha: Peerapon Boonyakiat/SOPA Images/IMAGO

Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina, mwenye miaka 76, aliingia madarakani mwaka 2009. Alituhumiwa kwa udanganyifu katika uchaguzi uliofanyika mwezi Januari. Mamilioni ya watu waliingia barabarani mwezi mmoja uliopita wakimtaka ang'oke madarakani. Mamia ya raia waliuwawa baada ya vikosi vya usalama kukabiliana nao ili kuzuia maandamano yaliyokuwa yakipinga mfumo wa utoaji ajira za umma.