1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana waanguasha utawala wa miaka 15 Bangladesh

6 Agosti 2024

Kiongozi wa Bangladesh Sheikh Hasina aliiokoa nchi kutoka kwenye utawala wa kijeshi, lakini utawala wake wa muda mrefu ulifikia ukomo baada ya waandamanaji kuivamia ikulu wakiipinga serikali kutoa upendeleo kwenye ajira.

https://p.dw.com/p/4j9RH
Bangladesh | Waandamanaji
Waandamanaji wakiwa wanapepeprusha bendera ya BangladeshPicha: Munir Uz Zaman/AFP/Getty Images

Maandamano nchini Bangladesh yalianza mnamo mwezi Julai kwanza kwa mikutano ya hadhara iliyoongozwa na wanafunzi wa vyuo vikuu kupinga upendeleo katika kugawa ajira kwenye utumishi wa umma na kisha maandamano ambayo hivi karibuni yaliongezeka na kuwa machafuko mabaya ambapo waandamanaji walimtaka kiongozi huyo aondoke madarakani.

Mashambulizi ya polisi na makundi ya wanafunzi wanaoiunga mkono serikali dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali yalilaaniwa kimataifa.

Bibi Hasina mwenye umri wa miaka 76, alishinda muhula wa tano kama waziri mkuuwa Bangladesh mnamo mwezi Januari 2024 katika uchaguzi ambao upinzani ulipinga matokeo yake kwa kusema haukuwa huru na wa haki.

Muda wa miaka 15 mfululizo aliokaa madarakani, Sheikh Hasina aliweza kuufufua upya uchumi wa Bangladesh, lakini pia utawala wake ulikabiliwa na matendo ya kukamatwa kwa wapinzani wengi wa kisiasa. Wakosoaji waliilaumu serikali ya Bangladesha kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu pamoja na mauaji ya wanaharakati wa upinzani.

Soma pia:Waziri Mkuu wa Bangladesh akimbia nchi

Sheikh Hasina ni binti wa mwanamapinduzi aliyeiongoza Bangladesh kupata uhuru, aliyekuwa Waziri Mkuu Sheikh Mujibur Rahman. Kiongozi huyo aliuawa pamoja na mkewe na wanawe wawili wa kiume katika mapinduzi ya mwaka 1975.

Kiongozi huyo wa Bangladeshi Sheikh Hasina alikimbia nchi na akarudi baada ya miaka sita uhamishoni na kuchukua hatamu za chama kilichoongozwa na baba yake cha Awami League, na alianzisha mapambano ya muongo mmoja ambayo yalijumuisha kuwekwa kwake kwenye kizuizi cha nyumbani kwa muda mrefu.

Safari ya kisiasa kuingia madarakani

Hasina aliungana na chama cha Khaleda Zia cha Bangladesh Nationalist Party (BNP) kilichomsaidia kumwondoa madarakani dikteta wa kijeshi Hussain Muhammad Ershad mwaka wa 1990.

Bangladesh | Dhaka | Sheikh Hasina
Aliekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh HasinaPicha: PID Bangladesh

Lakini walitofautiana na wakageuka kuwa wapinzani wakubwa katika siasa za Bangladesh. Hasina alihudumu kama waziri mkuu kwa mara ya kwanza mwaka 1996 lakini akashindwa na Zia miaka mitano baadaye.

 Wawili hao walifungwa kwa makosa ya rushwa mwaka 2007 baada ya mapinduzi ya serikali yaliyoungwa mkono na jeshi. Hata hivyo, mashtaka yaliyowakabili yalitupiliwa mbali na wakashiriki kwenye uchaguzi mwaka uliofuatia ambapo Sheikh Hasina alipata ushindi mkubwa na alienedelea kuwa madarakani tangu wakati huo hadi hapo jana alipoachia ngazi kutokana na shinikizo la waandamanaji.

Hatua ya serikali ya Bangladesh chini ya Sheikh Hasina ya kutowavumilia wapinzani ilizua chuki nyumbani na hali ya wasiwasi nchini Marekani na mahala kwingine duniani.

Soma pia:Waziri Mkuu wa Bangladesh Hasina awalaumu wapinzani wake kwa vurugu

Mnamo mwaka 2021 Marekani iliwawekea vikwazo maafisa wa kikosi maalum cha usalama nchini Bangladesh na maafisa wakuu saba wa kikosi hicho waliwekewa vikwazo kutokana na kukabiliwa na tuhuma nzito za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Sheikh Hasina aliendelea kusisitiza kwa waandamanaji wakati maandamano hayo yalipokuwa yanaongezeka kila uchao kwamba amelifanyia kazi taifa lake na alizuru maeneo katika jiji la Dhaka ambayo yaliharibiwa wakati wa machafuko mabaya ya mwezi uliopita.

Wafuasi wake wamemsifu Hasina kwa kuiongoza Bangladesh na kwa kuuimarisha uchumi wa nchi hiyo, kwa kiasi kikubwa kutokana na wafanyakazi wengi wanawake kuajiriwa kwenye kiwanda cha nguo zinazouzwa nje, sekta ambayo imechangia ukuaji wa uchumi.

Waziri Mkuu wa Bangladesh Hasina ajiuzulu