1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea urais Kongo watoa ahadi tele kuelekea uchaguzi mkuu

19 Desemba 2023

Wagombea urais nchini Kongo wametoa ahadi chungunzima kuelekea uchaguzi wa kesho Jumatano baada ya muda wa kufanya kampeni kukamilika rasmi jana katika hilo la Afrika ya Kati lenye idadi ya watu wapatao milioni 100.

https://p.dw.com/p/4aJx5
Uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mashine mpya ya kupigia kura itakayotumika katika uchaguzi mkuu wa KongoPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Ikiwa imesalia siku moja tu kwa uchaguzi huo kufanyika, tayari wagombea kadhaa wa urais wamejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho na kuwaacha wagombea 18 akiwemo rais wa sasa Felix Tshisekedi wakiwania nafasi hiyo ya juu.

Raia milioni 44 wa Kongo wamejiandikisha kama wapiga kura katika uchaguzi wa kesho wa urais, bunge na udiwani.

Soma pia: Tshisekedi: Uchaguzi wa Jumatano utafanyika katika mazingira ya kuaminika

Mbali na kunadi sera zao, wagombea hao walichukua muda mwingi kutupiana lawama na hata kauli nzito. Lakini miongoni mwa masuala yaliopewa kipau mbele ni suala la usalama. 

Wagombea wote wa urais wameahidi kumaliza vita na machafuko ya muda mrefu eneo la mashariki mwa Kongo.

Fayulu: Nikichaguliwa rais nitavunja uhusiano na Rwanda

Martin Fayulu, mmoja wa wagombea wa urais nchini Kongo akiwa jijini Kinshasa
Martin Fayulu, mmoja wa wagombea wa urais nchini KongoPicha: Reuters/B. Ratner

Rais Felix Tshisekedi amesema iwapo atachaguliwa kwa muhula wa pili ataliimarisha jeshi la nchi hiyo wakati Moise Katumbi akiahidi kuongeza mara dufu idadi ya wanajeshi na kupandisha mishahara yao.

Kwa upande wake, Martin Fayulu ameeleza kuwa, atavunja uhusiano wa kidiplomasia na nchi jirani ya Rwanda endapo atachaguliwa kuwa rais huku Denis Mukwege akiahidi kubadili mfumo mzima wa usalama.

Soma pia: Matamshi ya Cornelle Nangaa yaibuwa malumbano kati ya Kenya na DRC

Rais Tshisekedi amewashambulia hasa wapinzani wake na kuwaita kuwa ni wagombea wa nchi na maslahi za nje wakati wapinzani wake wakimkosoa kwa kushindwa kurejesha usalama na kuboresha mishahara ya wafanyakazi wa umma.

Wagombea wa upinzani pia wameikosoa tume ya uchaguzi CENI ambayo wamesema haijaweka wazi mchakato mzima wa uchaguzi.

Chama pekee ambacho hakikushiriki uchaguzi huo ni kile cha PPRD, chake rais wa zamani wa taifa hilo Joseph Kabila.