1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVisiwa vya Comoros

Wacomoro wasubiri matokeo ya uchaguzi wa rais

15 Januari 2024

Raia wa visiwa vya Comoro wanasubiri matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika siku ya Jumapili ambao rais aliye madarakani Azali Assoumani anatarajiwa kushinda muhula mwingine.

https://p.dw.com/p/4bEet
Uchaguzi wa Comoro 2024 | Moroni
Raia wa Comoro wakipiga kura.Picha: REUTERS

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea tangu kukamilika kwa upigaji kura jana jioni licha ya madai ya upinzani ya kuwepo kwa vitendo vya udanganyifu.

Kabla ya uchaguzi huo viongozi kadhaa wa upinzani kwenye taifa hilo la visiwa vya bahari ya Hindi, waliwatolea mwito wapiga kura kuususia .

Karibu wapiga kura 340,000 walikuwa wameandikishwa kushiriki uchaguzi huo kwenye taifa hilo lenye idadi kubwa ya waislamu na ambalo lilijitangazia uhuru kutoka ukoloni wa Ufaransa mnamo mwaka 1975.

Rais Assoumani anayechuana na wagombea wengine watano amesema anatumai kushinda katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi.

"Kuna imani kwamba nitashinda kwenye duru hii ya kwanza. Ni Mwenyezi Mungu ndiye atakayeamua na watu wa Comoro," alisema rais Assoumani baada ya kupiga kura kwenye kitongoji kimoja nje kidogo ya mji mkuu Moroni.

"Ikiwa nitashinda kwenye duru ya kwanza, tutaokoa muda na fedha," aliongeza kusema kiongozi huyo na kupuuza madai ya kuwepo hitilafu kwenye zoezi la uchaguzi.

Upinzani walia na dosari za uchaguzi na tuhuma za wizi wa kura

Uchaguzi wa Comoro 2024 | Rais Azali Assoumani
Rais Azali Assoumani anatarajiwa kushinda muhula mwingine madarakani.Picha: REUTERS

Wagombea wa upinzani wamelalamika kwamba kulikuwa na "udanganyifu" na "ujazaji masanduku karatasi za kura zilizokwishapigwa."

"Kama ilivyokuwa mwaka 2019, tunashuhudia udanganyifu (mwingine) kwenye uchaguzi ukifanywa na Azali Assoumani akishirikiana na jeshi," amesema mmoja ya wagombea wa kiti cha urais, Mouigni Baraka Said Soilihi, alipozungumza na waandishi habari.

Mwanasiasa huyo alikuwa ameambatana na wagombea wengine wanne wanaochuana na rais Assoumani.

Rais Assoumani -- ambaye amekuwa akiwakabili wakosoaji wake kwa mkono wa chuma ikiwemo kuwafunga jela na kuwalazimisha wengine kwenda uhamishoni-- amekanusha madai ya dosari kwenye uchaguzi huo.

Miongoni mwa dosari zilizotajwa ni hitilafu kwenye vituo vya kupigia kura ambazo amesema "hajazisikia" na kuhusu idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza, rais Assoumani alisema hilo limechangiwa na hali mbaya ya hewa husasani mvua iliyokuwa inanyesha jana Jumapili.

Zoezi la kuhesabu kura lilianza jioni baada ya vituo kufungwa. Matokeo ya uchaguzi huo wa jana yanatarajiwa ndani ya wiki hii.

Kura zahesabiwa kwa mishumaa na ulinzi mkali wa polisi

Uchaguzi wa Comoro 2024 | Kituo cha kura mjini Moroni
Upinzani unasema kulikuwa na dosari vituoni.Picha: Issihaka Mahafidhou/REUTERS

Kwenye maeneo mfano wa La Coulee, wilaya iliyo kusini mwa mji mkuu, kura zilikuwa zikihesabiwa kwa mwanga wa mshumaa huku ulinzi mkali wa polisi ukishuhudiwa nje ya vituo.

Msanii maarufu visiwani Comoro wa miondoko ya kufokafoka Cheikh MC, ambaye alikuwa mmoja ya waangalizi wa kuhesabu kura kwenye eneo hilo, amesema hakuvutiwa na zoezi lilivyokuwa linakwenda.

"Kwangu mimi, huu siyo uchaguzi. Tunashuhudia mchezo mchezo mchafu unaoweza kuleta balaa," amesema msanii huyo.

Kwa upande wake meneja wa kampeni za rais Assoumani, Houmed Msaidie ameyapinga madai yote ya kuwepo wizi au udanganyifu, akiwatuhumu upinzani kupiga kelele kwa "vitu vidogo na dhana zisizo na ukweli".

Rais Assoumani ambaye anatawala visiwa vya Comoro tangu mwaka 2016 alirefusha muhula wake madarakani kupitia mabadiliko tata ya katiba.

Mabadiliko ya katiba ya baada ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2019 yaliyoondoa sharti la nafasi ya urais kuwa ya kupokezana miongoni mwa visiwa vitatu vikubwa vinavyounda Jamhuri ya Comoro.

Wakati wa uchaguzi uliopita wa mwaka 2019,  waangalizi wa kikanda walisema kulikuwa na dosari nyingi na matokeo ya kura hiyo yalipungikiwa uhalali.