1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Comoro: Azali Assoumani apata ushindi wa kishindo

Daniel Gakuba
27 Machi 2019

Rais wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili. Matokeo yaliyochapishwa na tume ya uchaguzi jana jioni, yamempa Azali ushindi wa kishindo wa asilimia 66.77 ya kura.

https://p.dw.com/p/3FiLr
Wahlkampf auf den Komoren
Azali Assoumani, Rais wa Comoro ambaye ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa JumapiliPicha: AFP/Getty Images/Y. Ibrahim

Kwa ushindi huo Azali Assoumani amemwacha mbali mpinzani aliyekuja katika nafasi ya pili, Mahamoudou Ahamada ambaye kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa ameambulia asilimia 14.62 ya kura zilizopigwa, na kwa maana hiyo haitahitajika duru ya pili.

Lakini hata kabla ya matokeo hayo kutangazwa, tayari upinzani ulikuwa umekwishayapinga, ukidai kuwa upigaji kura uliandamwa na kasoro nyingi ambazo ziliripotiwa na tume ya uchaguzi. Upinzani huo ulizilinganisha kasoro hizo na mapinduzi dhidi ya serikali, na kutoa wito kwa umma kusimama kidete na kuipinga hali hiyo.Mahamoudou Ahamada alikwenda mbali na kuitaka jumuiya ya kimataifa kutoutambua ushindi wa Azali.

Azali ajipongeza, akiri kuwepo kasoro

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Azali Assoumani amekiri hitilafu zilijitokeza. ''Ni kweli makosa yalifanyika, lakini tunafurahi kwa sababu hali ingeweza kuwa mbaya zaidi.'' Alisema Azali na kuongeza kuwa wanajipongeza, na kumshukuru Mungu na Wakomoro.

Wahlkampf auf den Komoren
Mahamoudou Ahamada, mgombea aliyekuja katika nafasi ya piliPicha: AFP/Getty Images/Y. Ibrahim

''Kama nilivyosema, kipindi kigumu zaidi kiko mbele; ni kuijenga nchi na namwalika kila mmoja kushiriki.'' Ameongeza Azali Assoumani.

Zoezi la kuhesabu kura lilikumbwa na mivutano, ambayo ilihusisha matumizi ya nguvu za dola kuvunja maandamano ya upinzani juzi Jumatatu. Katika purukushani hizo watu 12 walijeruhiwa na polisi waliotumia risasi za mpira kuwazuia wafuasi wa wagombea wa upinzani walioandamana katikati mwa mji mkuu, Moroni.

Wapinzani wadai sio uchaguzi, bali mapinduzi

Mgombea urais waliyekuja katika nafasi ya tatu Mwinyi-Baraka Said Soilihi, amesema hawautambui mchakato mzima.

Amesema, ''Kwetu sisi kilichofanyika ni mapinduzi badala ya uchaguzi. Mapinduzi yaliyopangwa na Azali na timu yake kwa kulishirikisha jeshi. Tuliwaona wanajeshi wakibeba visanduku vya kura katika vituo vingi, hususani katika visiwa vya Anjouan na Moheli.''

Komoren Auseinandersetzung auf der Insel Anjouan
Zoezi la uchaguzi liligubikwa na mivutanoPicha: Getty Images/AFP/Y. Ibrahim

Watu 300,000 kati ya wakazi wote 800,000 wa Comoro walikuwa na haki ya kupiga kura. Wapinzani wakuu wa Rais Azali, akiwemo Ahmed Abdallah Sambi walizuiliwa na mahakama kuu kugombea, kwa tuhuma za ufisadi.

Mkurugenzi wa kampeni ya Azali Assoumani, Houmed Msaidie ametupilia mbali ukosoaji wa wapinzani, akiwashutumu kuwa na nia ya kuweka mazingira ya hofu ili kuhujumu uhalali wa mfumo wa uchaguzi, na amewashauri walio na malalamiko kuyapeleka katika taasisi zinazohusika.

Azali Assoumani aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1999, na baadaye alishinda uchaguzi wa rais ulioandaliwa mwaka 2002 na wa mwaka 2016.

AFPE,RTRE