1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Comoro Ahmed Sambi afungwa maisha

28 Novemba 2022

Mahakama visiwani Komoro imemuhukumu kifungo cha maisha rais wa zamani, Ahmed Abdallah Sambi, baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya uhaini yanayohuishwa na kuuza hati za kusafiria za nchi hiyo kwa raia wa kigeni.

https://p.dw.com/p/4KBr2
Komoren Moroni | Ex-Präsident Ahmed Abdallah Sambi vor Gericht
Rais wa zamani Ahmed Abdallah Sambi (mwenye juba) akisindikiza na askari wakati akiwasili mahakamani mjini Moroni, Novemba 21, 2022. Sambi amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Mei 2018.Picha: Ibrahim Youssouf/AFP/Getty Images

Sambi, mwenye umri wa miaka 64, na hasimu mkubwa wa Rais Azali Assoumani, amehukumiwa na Mahakama Maalum ya Usalama wa Taifa, chombo maalum kilichowekwa na ambacho hukumu zake haziwezi kukatiwa rufaa.

Rais wa mahakama hiyo, Omar Ben Ali alisema wakati wa kusoma hukumu hiyo mchana wa leo, na hapa namnukuu: "Sambi anahukumiwa kifungo cha maisha. Mahakama hii inaamuru mali zake zote kutaifishwa kwa maslahi ya umma." Mwisho wa kumnukuu.

Soma pia: Komoro yataka rais wa zamani ahukumiwe kifungo cha maisha

Ben Ali alisema pia kuwa mahakama hiyo maalum imemuondoshea rais huyo wa zamani haki ya kupiga na kupigiwa kura kushikilia ofisi yoyote ya umma.

Ahmed Abdallah Mohamed Sambi Präsident Komoren
Rais Ahmed Abdallah Sambi amefungwa maisha kwa uhaini mkubwa.Picha: picture-alliance/ dpa

Sambi alihukumiwa wakati mwenyewe akiwa hayupo mahakamani baada ya kukataa kuhudhuria vikao vya kesi hiyo.

Aliwahi kushiriki kwa muda mfupi wakati kesi ilipotajwa kwa mara ya kwanza, ambapo mawakili wake walimuomba jaji kujitowa kwani aliwahi kuwa sehemu ya jopo la waendesha mashitaka. Ombi hilo lilikataliwa.

Kabla ya kuacha kuhudhuria vikao vilivyoendelea vya kesi hiyo, Sambi alisema kwamba uundwaji wa mahakama yenyewe ni kinyume na sheria na kwamba asingependa kuhukumiwa na mahakama ya aina hiyo.

Bintiye Sambi: Ni jopo la dhihadaka

Akizungumza na shirika la habari la AFP muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutangazwa, binti wa Sambi, Tisslame Sambi, alisema kwamba hukumu yenyewe inalingana kabisa na kile ambacho wamekuwa wakikisema tangu awali.

Soma pia: Comoro: Azali Assoumani apata ushindi wa kishindo

Tisslame aliongeza na hapa namnukuu: "Jopo la dhihaka kwenye mahakama inayoongozwa na wajumbe wa serikali ambayo inatowa hukumu ya kifungo cha maisha kwa mpinzani mkubwa kabisa wa utawala uliopo madarakani." Mwisho wa kumnukuu.

Sambi, aliyeliongoza taifa hilo dogo la Bahari ya Hindi baina ya mwaka 2006 na 2011, alipitisha sheria inayoruhusu uuzaji wa hati za kusafiria kwa bei ya juu, kupitia mpangokm ulioitwa bidoon - neno la Kiarabu linalomaanisha maelfu ya watu ambao hawawezi kupata haki ya uraia.

Libyen Gipfelkonferenz der Arabischen Liga
Rais Sambi akiwa na kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Ghadafi, Machi 26, 2010.Picha: AP

Kiongozi huyo wa zamani alituhumiwa kufanya ubadhirifu wa mamilioni ya dola kupitia mpango huo.

Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, hasara iliyopatikana kwenye hazina kuu ya nchi ilifikia dola bilioni 1.8 za Kimarekani - zaidi ya pato jumla la nchi hiyo masikini.

Soma piaRais wa Comoro amesitisha korti ya katiba 

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Ali Mohamed Djounaid, aliiambia mahakama wiki iliyopita kwamba Sambi alilisaliti jukumu alilopewa na raia wa Komoro, na akaiomba mahakama imfunge kifungo cha maisha.

Wakili Eric Emmanuel Sossa aliyewakilisha upande wa serikali alisema serikali ya Sambi iliwapa majambazi haki ya kuuza uraia wa Komoro kama njugu sokoni, lakini wakili wa Sambi, Jean-Gilles Halimi, amesema hakuna ushahidi wowote wa fedha zilizopotea ama akaunti za benki ambazo ziliwasilishwa mahakamani kuonesha jinsi ufisadi huo ulivyofanyika.

Chanzo: AFP