1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wauteka mji wa Kanyabayonga

Josephat Charo
29 Juni 2024

Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa kundi la M23 wameuteka mji wa kimkakati wa Kanyabayonga katika eneo linalokabiliwa na machafuko la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

https://p.dw.com/p/4hfS4
Waasi wa kundi la M23 wakiwa huko Kibumba
Waasi wa M23 wakiwa wamesimama na silaha zao huko Kibumba, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Desemba 23, 2022Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mji wa Kanyabayonga umekuwa mikononi mwa waasi wa M23 tangu Ijumaa jioni," alisema afisa tawala kwa masharti ya kutotajwa jina.

Mji huo unapatikana eneo la kaskazini la mzozo katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ambalo limekabiliwa na machafuko tangu 2021 wakati M23 waliopanza tena kampeni yao ya mashambulizi ya silaha katika eneo hilo. Mji huo pia unachukuliwa kuwa njia muhimu kuelekea vituo vikubwa vya kibiashara mjini Butembo na Beni upande wa kaskazini.

Mji wa Kanyabayonga ni nyumbani kwa watu zaidi ya 60,000 pamoja na maalfu ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao katika miezi ya hivi karibuni, wakifukuzwa kutoka kwenye nyumba zao na waasi wanaosonga mbele.

Soma pia: Mapigano yaongezeka mashariki mwa Congo

Mji wa Kanyabayonga unapatikana eneo la Lubero, himaya ya nne katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambayo kundi la M23 limefanikiwa kuingia baada ya Rutshuru, Nyiragongo na Masisi.

"Watu wako huko hasa wale ambao walihamia kutoka eneo la Rutshuru hadi Lubero," aliongeza kusema afisa tawala. "Hawana tena mahali pa kwenda, ni ukiwa kamili, umma umechoka," akaongeza kusema.

Ramani ya eneo la mashariki mwa Congo
Ramani ya eneo la mashariki mwa Congo

Mkazi mmoja ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba waasi wa M23 waliwaomba wakaazi waendelee kukaa Kanyabayonga wakati wa mkutano uliofanyika katikati ya mji uliofanywa na msemaji wa kundi hilo, Willy Ngoma Jumamosi.

"Watafika Kinshasa, tutaendelea kukimbia hadi umbali gani?" aliuliza mkazi huyo, akiongeza kwamba waasi "wanaahidi amani".

"Tunaona ongezeko la watu wasio na makazi kutoka Miriki, Kirumba na Luofu kuelekea kaskazini," mtawala wa kijeshi wa eneo la Lubero, Kanali Alain Kiwewa, alisema. "Ni hali inayotutia wasiwasi," aliongeza.

Mapigano yaongezeka

Duru katika eneo hilo zimeliambia shirika la habari la AFP kwamba mapigano kati ya vikosi vya Congo na waasi yalikuwa yanaongezeka katika maeneo yanayouzunguka mji wa Kanyabayonga. Watu walio nje ya mji huo pia walishuhudia mapigano hayo.

"Usiku kucha risasi zilirindima," alisema kiongozi wa vijana katika mji wa Kayna unaopatikana kiasi kilometa 17 kaskazini mwa Kanyabayonga. Kiongozi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wale ambao walikuwa wamekuja mjini humo kutokea Kanyabayonga walilala nje usiku kucha na walijawa na hofu. "Hatufahamu tena ni mtakatifu yupi wa kumgeukia," alisema.

Mjini Kirumba, kiasi kilometa 25 kutoka Kanyabayonga, umma uko katika hali ya taharuki, alisema kiongozi mmoja wa shirika la kijamii kwa masharti ya kutotajwa majina. "Hatuwezi kusogea kwenda kokote, tutakwenda wapi? Hatujui kwa kwenda," alisema.

Makabiliano yanasababisha raia kuyakimbia makazi yao, ilisema afisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu katika ripoti yake ya kila mwezi iliyochapishwa siku ya Ijumaa.

"Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanayotoa msaada kwa watu waliokimbia makazi yao yamesitisha shughuli zao kwa sababu za kiusalama," ilisema ripoti hiyo.

Chanzo: AFP