1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaongezeka mashariki ya Kongo

29 Juni 2024

Mapigano yameongezeka katika mji mmoja wa kimkakati mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vya eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4hent
Machafuko Mashariki ya Kongo
Waasi wa M23 walianzisha tena harakati zao za mapigano katika mkoa wa Kivu KaskaziniPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Makabiliano ya jana Ijumaa yalitokea katika mji wa Kanyabayonga, ulioko kaskazini mwa uwanja wa mapambano katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Mkoa huo umekumbwa na machafuko tangu mwaka wa 2021 wakati M23 walipoanzisha tena harakati zao za mapigano katika eneo hilo.

Mji wa Kanyabayonga unazingatiwa kuwa mlango wa kuingia Butembo na Beni katika upande wa kaskazini, ambazo ni ngome za kabila la Nande na vituo muhimu vya kibiashara. Kanyabayonga, ni mji wenye wakazi 60,000, na uko karibu kilomizta 100 kutoka mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, ambao pia umezingirwa na waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda.

Waasi wa M23 walisonga mbele kuelekea Kanyabayonga katika wilaya ya Lubero, ikiwa ni eneo la nne la mkoa huo, ambalo kundi hilo limeingia baada ya Rutshuru, Nyiragongo na Masisi. Afisa mmoja wa utawala katika eneo hilo amesema mapigano yanaendelea katika eneo la Kanyabayonga na viunga vyake, lakini jeshi bado liko huko.