1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yakanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23

17 Juni 2024

Jeshi la Uganda limekanusha madai kwamba linatoa msaada kwa wapiganaji wa M23 ambao wanaendesha harakati zao Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4h8YG
Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni Picha: Darko Vojinovic/AP Photo/picture alliance

Naibu msemaji wa jeshi la Uganda Luteni Kanali Deo Akiiki ameitaja ripoti iliyotolewa na kundi maalum la wataalam wa Umoja Mataifa kuwa yenye taarifa za kupotosha, na  kuonyesha uzembe katika kufanya uchunguzi bila kufuatilia hali halisi ya mambo.

Madai hayo yametolewa wakati wimbi jipya la mzozo likifukuta mashariki mwa Congo ambapo zaidi ya raia 150 wameuawa katika mashambulizi yanayofanywa na waasi wa ADF  katika kipindi cha mwezi mmoja.

Wiki iliyopita, ripoti hiyo kuhusiana na amani na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ilielezea kuwa Uganda inatoa msaada kwa wapiganaji wa M23 pamoja na kundi lingine lijulikanao kama Alliance Fleuve Congo (AFC). 

Soma pia:Jimbo la Kivu Kusini linahitaji kama dola milioni 56 kujijenga upya
Kulingana na ripoti hiyo, licha ya  wapiganaji wa M23  kuwekewa vikwazo na Umoja Mataifa, Uganda imewaruhusu viongozi wao husafiri nchi za nje wakipitia uwanja wa kimataifa wa Entebbe.

Ripoti hiyo aidha inadai kuwa mwanahabari maarufu wa Uganda Andrew Mwenda ndiye hushughulikia masuala  ya kidiplomasia ya wapiganaji wa M23 na mataifa ya kigeni.

Mwanahabari huyo ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya Jarida la Independent amethibitisha kuwa amewahi kukutana na viongozi wa M23. Ila akaelezea kuwa ilikuwa ni katika mazingira ya kupata maudhui ya habari za chapisho lake.