1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi waomboleza kifo cha waziri Mkuu mstaafu Shinzo Abe

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
8 Julai 2022

Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe amefariki dunia hospitalini, alikopelekwa baada ya kupigwa risasi wakati anahutubuia kwenye mkutano wa kampeni katika mji wa Nara magharibi mwa Japan.

https://p.dw.com/p/4Dqmk
Japan | Wahlen | Shinzo Abe
Picha: Kyodo/picture alliance

Waziri mkuu wa sasa wa Japan Kishida alitoa taarifa juu ya kushambuliwa kwa Abe mapema leo asubuhi. Shinzo Abealikuwa anahutubia kwenye mkutano wa kampeni kwa niaba ya chama chake cha Liberal Demokratic. Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Japan, Shinzo Abe aliyekuwa na umri wa miaka 67 alizimia mara tu baada ya kushambuliwa na alionekana akivuja damu, kabla ya kupelekwa haraka hospitali ambapo alifariki.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida
Waziri Mkuu wa Japan Fumio KishidaPicha: Kyodo/imago images

Polisi wamesema wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 41 wanayemshuku kuhusika na tukio hilo. Shirika la habari la Japan NHK limemnukuu mtuhumiwa huyo Tetsuya Yamagami aliyewaambaia polisi kwamba alidhamiria kumuua Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe kwa sababu hakuridhika nae.

Waziri Mkuu wa sasa wa Japan Fumio Kishida, amelaani vikali shambulizi hilo dhidi ya Abe lililotokea katika mji wa Nara ulio magharibi mwa Japan huku watu wa Japan na viongozi wa dunia wakionesha kushtushwa na mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe katika nchi ambayo ni nadra sana kuwepo vurugu za kisiasa na kuna sheria kali za kudhibiti matumizi ya bunduki. Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema kuuawa kwa Shinzo Abe, ni kitendo kisichoweza kusameheka.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Thomas Imo/photothek/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameelezea kushtushwa kwake na shambulio dhidi ya waziri mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ameshtushwa sana na shambulio lililosababisha kifo cha Shinzo Abe. Amesema mawazo yako pamoja na familia, raia wa Japan na marafiki wa karibu wa waziri mkuu mkuu huyo wa zamani na kwamba Ufaransa inasimama na watu wa Japan katika wakati huu mgumu.

Abe alikua waziri mkuu wa Japan aliyekaa uongozini kwa muda mrefu zaidi kutoka mwaka 2006 hadi mwaka 2020. Kufikia wakati wa majira ya joto mnamo mwaka wa 2020, umaarufu wake ulisambaratika kutokana na jinsi alivyoushughulikia mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 na pia kutokana na msururu wa kashfa zikiwemo za kukamatwa waziri wake wa zamani wa sheria.

Waziri Mkuu wa zamani wa Japan aliyeuawa kwa kupigwa risasi Shinzo Abe
Waziri Mkuu wa zamani wa Japan aliyeuawa kwa kupigwa risasi Shinzo AbePicha: Kyodo/picture alliance

Alijiuzulu mwaka huo wa 2020 kwa sababu ya ugonjwa, lakini alidumisha uwepo wake kwenye maswala ya kisiasa. Moja ya malengo yake makuu yalikuwa kuboresha ulinzi wa nchi yake na katiba ili Japan iweze kushiriki katika shughuli za kijeshi za kimataifa.

Mtuhumiwa aliyekamatwa anadaiwa kumfyatulia risasi mbili Abe kutokea nyuma na alitumia bunduki iliyotengenezwa nyumbani wakati Abe akitoa hotuba ya kampeni ya uchaguzi mjini Nara.