1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Shinzo Abe afariki dunia baada ya kupigwa risasi

Sylvia Mwehozi
8 Julai 2022

Waziri mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe amefariki baada ya kupigwa risasi wakati akiwa katika mkutano wa kampeni katika mji wa Nara siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4DqLo
Japan l Ex-Regierungschef Shinzo Abe ist tot
Picha: Jorge Silva/REUTERS

Shirika la habari la Japan NHK limeonesha video ya Abe akitoa hotuba ya kampeni nje ya kituo cha treni wakati risasi mbili zilipofyatuliwa, na baadaye picha hizo zilifichwa kwa muda na ndipo maafisa wa usalama walionekana wakikabiliana na mshambuliaji.

Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida amelaani vikali shambulio hilo ambalo amelitaja kuwa shambulio dhidi ya demokrasia ya Japan. Kishida amelazimika kukatisha kampeni zake katika mji wa kaskazini wa Yamagata na kurejea mjini Tokyo.

Afisa mmoja wa hospitali alisema awali kuwa Abe alionekana kuwa katika hali ya mshtuko wa moyo wakati akipelekwa hospitalini kwa ndege, lakini awali alikuwa na fahamu.

Polisi walisema mwanamume mwenye umri wa miaka 41 anayeshukiwa kutekeleza tukio hilo la risasi amekamatwa. Shirika la habari la Japan la NHK lilimnukuu mshukiwa, aliyetambulika kwa jina la Tetsuya Yamagami, akiwaambia polisi kwamba hakuridhika kwasababu alitaka kumuua Abe.