1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi walaumu hujuma kwa uvujaji wa Nord Stream 1 na 2

28 Septemba 2022

Umoja wa Ulaya umesema unashuku uharibifu uliotokea kwenye mabomba mawili yanayosafirisha gesi kupitia chini ya bahari ulitokana na hujuma, na kuonya kulipiza mashambulizi yoyote dhidi ya mitandao ya nishati ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/4HSRi
Deutschland | Gas Pipeline Nord Stream 1
Picha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel, amesema katika taarifa kwa niaba ya mataifa 27 wanachama wa  jumuiya hiyo, kwamba taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa uvujaji kwenye mabomba hayo ulitokana na kitendo cha makusudi, na kusisitiza kuwa uvurugaji wowote wa kudhamiria wa miundombinu ya nishati ya kanda hiyo haukubaliki na utakabiliwa na majibu makali ya pamoja.

Soma pia: Gesi ya Urusi yazidi kupungua kuingia Ulaya

Ikulu ya Urusi, Kremlin, ilisema Jumanne kuwa mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 yalikuwa yameharibiwa na uwezekano wa hujuma hauwezi kuondolewa. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, alisema upande wa Urusi una wasiwasi mkubwa kuhusu uharibifu wa mabomba hayo, na kuongeza kuwa hali yake itaathiri usalama wa nishati wa bara zima la Ulaya.

Wataalamu wa uchunguzi wa matetemeko ya ardhi waliripoti Jumanne kwamba milipuko ilitikisa bahari ya Baltic kabla ya kugunduliwa kwa uvujaji huo usio wa kawaida kwenye mabomba hayo yanayoruhusu gesi kusafirishwa hadi Ujerumani bila kupitia Ukraine au Poland.

Infografik - Nord Stream 2 safety zone around the island of Bornholm - EN
Ramani inayoonesha maeneo ulikotokea uvujaji kwenye mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na 2.

Uharibifu huo unamaanisha kwamba huenda yasiweze kusafirisha gesi yoyote kwenda Ulaya msimu huu wa baridi, hata kama nia ya kisiasa ya kuyarudisha itakuwepo, kwa mujibu wa wachambuzi.

Soma pia: Ujerumani yakataa maelezo ya Urusi kuhusu Nord Stream 1

Uvujaji kwenye mabomba hayo uligunduliwa nje ya kisiwa cha Denmark cha Bornholm kilichoko bahari ya Baltic, na waziri mkuu wa Denmark Mette Frederiksen amesema tathmini ya serikali inaonesha wazi kuwa ni hatua za maksudi na siyo ajali. Lakini alisema hakukuwa na taarifa kuashiria nani yalikuwa nyuma ya hujuma hiyo.

"Siyo jambo la kawaida," alisema waziri mkuu Frederiksen. "Kuna maeneo matatu yanayovuja, yakiwa hata na umbali kati yake. Na hii ndiyo sababu ni vigumu kudhani kwamba kinachotokea ni tukio lililotokea tu kwa wakati mmoja."

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO, Jens Stoltenberg pia ameuelezea uvujaji huo kuwa kitendo cha hujuma, baada ya mkutano kwenye makao makuu ya muungano huo wa kijeshi mjini Brussels, na waziri wa ulinzi wa Denmark Morten Bödskov.

Dänemark | Gasleck in der Pipeline Nord Stream 2
Picha ya jeshi la Denmark inayoonyesha uvujaji wa gesi kwenye bomba la Nord Stream 2 katika kisiwa cha Bornholm, Denmark, Spetemba 27,2022.Picha: Danish Defence/handout/AA/picture alliance

Bodskov amesema inaweza kuchukuwa hadi wiki mbili kabla ya mabomba hayo kukaguliwa, kutokana na presha ndani yake na kiwango cha gesi kinachovuja.

Soma pia: Urusi imelifunga bomba la gesi inayoingia Ujerumani

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, amesema Marekani iko tayari kuwasaidia washirika wake wa Ulaya kuhusu usalama wa nishati kufuatia uvujaji huo, na kuogeza kuwa wanashirikiana kwa karibu kutatua suala la usalama wa nishati barani Ulaya na kote duniani.

Ukraine imeishutumu urusi kwa kusababisha uvujaji huo, ikisema vitendo hivyo ni sawa na shambulizi la kigaidi.

Chanzo: Mashirika