1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa ulimwengu waanza kuhutubia mkutano wa COP28

Sylvia Mwehozi
1 Desemba 2023

Viongozi wa dunia wamewasili Dubai kwa mazungumzo ya mkutano wa kimataifa wa mazingira wa COP28, chini ya shinikizo la kuongeza juhudi za kupunguza ongezeko la joto duniani.

https://p.dw.com/p/4Zf43
Mkutano wa COP28 Dubai
Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan (katikati)akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa ulimwengu Picha: Amr Alfiky/Reuters

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan amewapokea viongozi wa ulimwengu akiwemo Mfalme Charles wa III wa Uingereza, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na viongozi wengine waliowasili leo Dubai.

Mkutano wa COP28 ulianza jana AlhamisI kwa mafanikio ya mapema wakati mataifa yalipokubaliana kuanzisha mfuko maalum wa "hasara na uharibifu"kwa nchi zilizoathirika na majanga ya asili. Lakini wajumbe wanakabiliwa na wiki mbili za mazungumzo magumu juu ya masuala kadha ambayo kwa muda mrefu yamekuwa kizungumkuti katika mazungumzo ya mazingira, kuanzia na mustakabali wa mafuta, gesi na makaa ya mawe.  

Mkutano wa COP28 Dubai | Mfalme Charles III
Mfalme Charles wa III wa Uingereza akihutubia hadhira ya viongozi wa ulimwengu katika mkutano wa COP28Picha: Rafiq Maqbool/AP

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman ambaye nchi yake ni mzalishaji mkuu wa mafuta, na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, ambaye miji yake mikubwa inasongwa na uchafuzi wa hali hewa mara kwa mara, ni miongoni mwa viongozi zaidi ya 130 wa dunia wanaotarajiwa kuhutubia mkutano wa COP28 ndani ya siku mbili zijazo.

Soma uzinduzi wa COP28: Mkutano wa COP28 wafunguliwa huko Dubai

Hata hivyo viongozi wa mataifa mawili makubwa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa hewa chafuzi ya kaboni ambayo inachangia zaidi ya asilimia 44 ya uchafuzi wa hewa duniani, Rais Joe Biden wa Marekani na Rais wa China Xi Jinping hawatokuwepo. Xi na Biden watakosa mkutano huo ikiwa ni wiki mbili baada ya kutangaza makubaliano ya pande mbili ya kusaidia kupunguza uzalishaji wa Methane. Viongozi hao watawakilishwa na manaibu wao, Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris na Waziri Mkuu wa kwanza wa China Ding  Xuexiang.

COP28 Dubai
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28)Picha: Mahmoud Khaled/Reuters

Mfalme Charles wa III wa Uingerezatayari amehutubia hadhira ya viongozi wa ulimwengu hii leo akisema kwamba mazungumzo ya mwaka huu yanapaswa kuwa na dhamira ya kweli ya kuleta mageuzi.

"Ninasali kwa moyo wangu wote kwamba COP28 utakuwa mkutano mwingine muhimu kuelekea hatua thabiti za mageuzi katika wakati ambao tayari, kama wanasayansi walivyokwisha kuonya kwa muda mrefu, tunashuhudia kufikia hatua za kutisha," alisema Mfalme Charles.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kabla ya kuhutubia mkutano huo amenukuliwa akisema kuwa ulimwengu hauwezi kuiokoa sayari inayowaka kwa bomba la moto la nishati ya visukuku, akiongezea kuwa kikomo cha nyuzi joto 1.5 kinawezekana tu endapo dunia itaacha matumizi ya nishati itakanayo na mafuta ya visukuku.