1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa COP28 wafunguliwa huko Dubai

Saleh Mwanamilongo
30 Novemba 2023

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi unafunguliwa huku mataifa yakihimizwa kuongeza kasi ya kuchukua hatua za kupambana na ongezeko la joto duniani na kukomesha nishati ya visukuku.

https://p.dw.com/p/4Zbwj
Viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani wamejumuika pamoja huko Dubai, kushiriki mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi  COP28
Viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani wamejumuika pamoja huko Dubai, kushiriki mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi COP28Picha: Jewel Samad/AFP/Getty Images

Wakati viongozi wa kimataifa wakikusanyika Dubai kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi Duniani, wajumbe wanatarajia kufikia makubaliano ya mapema kuhusu juhudi za kukabiliana na majanga.

Mazungumzo ya wiki mbili yanayofanyika mwaka huu katika jiji hilo la Ghuba lililong'aa yanakuja katika wakati muhimu, huku uzalishaji wa hewa ukaa bado ukiongezeka na mwaka huu unatarajiwa kuwa na viwango vya juu vya joto zaidi katika historia ya binadamu.

Mfalme wa Uingereza Charles III, viongozi wa dunia, wanaharakati na watetezi wa mazingira ni miongoni mwa zaidi ya watu 97,000 wanaotarajiwa kuhudhuria kile kinachotajwa  kuwa mkutano mkubwa zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi wa aina yake.

''Kitu pekee ambacho bado kinakosekana ni utashi wa kisiasa''

Umoja wa Mataifa na wenyeji, Umoja wa Falme za Kiarabu wanasema mazungumzo haya, ya mkutano wa COP28, yatakuwa muhimu zaidi tangu yale ya Paris mwaka 2015. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mkutano huo unapaswa kuwa na lengo la kukomesha kikamilifu kwa nishati ya visukuku.

"Kitu pekee ambacho bado kinakosekana ni utashi wa kisiasa. Na ninamaanisha, hii ndiyo sababu mkutano wa COP ni muhimu, kuwafanya watu waelewe kuwa tunasonga katika mwelekeo mbaya sana.'', alisema Guterres.

Kabla ya kuongeza kuwa : ''Ikiwa hakuna kitakachofanyika tunaelekea nyuzi joto tatu. Na hiyo itakuwa janga kubwa.Lakini tuna uwezo, teknolojia na uwezo na pesa kwa sababu pesa zinapatikana, ni suala la kuhakikisha kuwa zinaingia katika mwelekeo sahihi kufanya kile kinachohitajika." 

Matarajio ya nchi za Afrika

Masuala ya ufadhili kwa nchi masikini ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi linatarajiwa pia kujadiliwa
Masuala ya ufadhili kwa nchi masikini ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi linatarajiwa pia kujadiliwa Picha: Giuseppe Cacace/AFP

Wanasayansi wanasema ulimwengu hauko kwenye njia ya kufikia malengo ya kupunguza gesi chafu kwa nyuzi joto 1.5 na mataifa lazima yapunguze kwa kasi na kwa kina zaidi utoaji wa hewa chafu ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabia nchi.

Afrika itegemee nini kutoka mkutano huu wa COP 28 ?  Frank Luvanda, ni katibu mtendaji wa shirika la Mazingira Network, nchini Tanzania ( MANET).

''Ni matarajio yetu makubwa kwamba mkutano huu wa COP28 utaimarisha makubaliao yamekwisha fanyika hapo awali, hasa ya kuzisaidia nchi za Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.'', alisema Luvanda.

Siku ya Ijumaa na Jumamosi, Marais na wakuu nchi wapatao 140 wanatarajiwa kueleza azma yao baada ya mwaka mmoja wa mafuriko makubwa, majanga ya moto na vimbunga  kote ulimwenguni. Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis alilazimika kughairi kushiriki mkutano huo dakika za mwisho kutokana na homa.