1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 kuisaidia zaidi Ukraine, kuishinikiza zaidi Urusi

28 Juni 2022

Katika kuhitimisha mkutano wao wa kilele wa siku tatu, viongozi wakuu wa G7 wamekubaliana kuweka ukomo wa bei kwenye mafuta ya Urusi na kutoa mabilioni katika msaada wa chakula ili kuepusha mzozo wa njaa kutokana na vita.

https://p.dw.com/p/4DNbR

Katika tamko la kufunga mkutano wa kilele wa G7, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, mwenyeji wa mkutano huo, alismea mataifa saba yanayoongoza kiuchumi duniani yanasimama pamoja katika kuiunga mkono Ukraine na kwamba mataifa ya G7 yatapandisha gharama ya vita kwa Urusi.

Viongozi hao wa G7 walihitimisha mkutano wao wa kilele wa siku tatu siku ya Jumanne katika eneo la milima ya Alps la Bavaria, kwa ahadi za kuishinikiza zaidi Urusi luhusiana na vita vyake nchini Ukraine, huku wakishughulikia pia mzozo unaofukuta wa ukosefu wa chakula uliosababishwa na kuzuwiwa kwa ugavi wa chakula.

Rais wa Urusi Vladmir Putin "hapaswi kushinda vita hii."  "Tutaendeleza kampeni ya kupandisha gharama za kiuchumi na kisiasa za vita hivi," aliongeza Scholz. "Kuna njia moja tu ya kutoka: kwa Putin kukubali kwamba mpango wake nchini Ukraine hautofanikiwa," alisema Scholz.

Soma pia: Viongozi wa G7 waazimia kukabiliana na kitisho cha njaa duniani

"Tunataka Ukraine iweze kulinda mamlaka yake, uhuru na mustakabali wa demokrasia," alisema Scholz. "Tunaiunga mkono nchi hiyo katika kujitetea na kuipatia matumaini ya wakati ujao," aliongeza.

"Jukumu linalofuata ni kuona kwamba vita hivi vinafikia mwisho, na Urusi inaondoa wanajeshi wake," alisema Kansela Scholz.

Vita vya Urusi nchini Ukraine vinatazamiwa pia kuugubika mkutano wa jumuiya ya kujihami NATO mjini Madrid, ambako wengi wa viongozi wa G7 wataelekea kutokea Ujerumani.

Deutschland | G7 Gipfel auf Schloss Elmau
Viongozi wa G7 wamekutana katikati mwa mizozo kadhaa iliyosababishwa na vita vya Urusi nchini Ukraine.Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Akizungumza baada ya kansela Scholz, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema Urusi "haiwezi na haipaswi kushinda" vita nchini Ukraine.

"Hivi sasa, ni wazi, Uvamizi wa Urusi kwenye ardhi ya Ukraine una lengo moja - kujisalimisha kwa Ukraine," alisema Macron, na kuongeza kuwa G7 itaisaidia Ukraine," kadiri itakavyohitajika na kwa nguvu inayohitajika."

Mpango kabambe kwa ajili ya Ukraine

Scholz alisema Ujerumani inashirikiana na halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya kuandaa mkutano wa ujenzi mpya wa Ukraine baada ya vita.

"Tumejizatiti kabisaa kusaidia ujenzi mpya wa Ukraine kupitia mkutano wa kimataifa wa ujenzi mpya na mpango wa kimataifa wa ujenzi mpya, ambao utabuniwa na kutekelezwa na Ukraine kwa uratibu wa karibu na washirika wa kimataifa," alisema Kansela wa Ujerumani.

"Tunahitaji mpango kabambe kwa ajili ya Ukraine, unapaswa kupangiliwa vyema na kuendelezwa, hicho ndicho tumejipanga kukifanya," aliongezea Scholz, akimaanisha juhudi zilizoongozwa na Marekani kuijenga upya Ulaya baada ya Vita kuu vya pili vya Dunia.

Soma zaidi: Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"

"Haitahusu juhusu za miaka michache, itakuwa juu ya miaka ingi," aliongeza, akiutaja ujenzi mpya wa Ukraine kuwa "jukumu babkubwa" kwa dunia.

Mpango wa kudhibiti bei za mafuta ya Urusi

Maafisa wa Marekani wakizungumza na waandishi habari kwa sharti la kutotajwa majina, walisema mataifa ya G7 yamekubaliana kubuni mfumo wa kuweka ukomo kwenye mafuta ya urusi ili kupunguza faifa ya Moscow kutokana na bei zinazozidi kupanda za mafuta.

Viongozi wa G7 watazipa jukumu wizara kufanya kazi haraka kuelekea kuanzisha, kushauriana na mataifa mengine na sekta binafsi katika juhudi za kuweka ukomo wa bei kwenye mafuta ya Urusi," alisema afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani.

G7 Gipfel Schalte mit Selenskyj
Wakuu wa mataifa ya G7 na Ulaya wameahidi kuisaidia Ukraine bila kuchoka, na kuipandishia Urusi gharama ya vita.Picha: Tobias Schwarz/AFP

"Tutachunguza hatua zaidi ili kuizuwia Urusi kufadika kutokana na vita vyake vya uvamizi. Tunapoondoa mafuta ya Urusi kwenye masoko yetu ya ndani, tutatafuta kubuni njia zinazokidhi malengo ya kupunguza mapato ya Urusi kutokana na gesi ya kaboni, na kusaidia utulivu wa masoko ya kimataifa ya nishati," ilisema taarifa ya mwisho ya viongozi wa G7.

Mpango huo utahusisha huduma za kifedha, bima na usafirishaji kwa bei iliyopunguzwa kwa mafuta ya Urusi, na kuwalazimisha wale wanaotumia huduma hizi kulipa bei iliyowekwa, bei ya chini ya mafuta hayo, kulingana na shirika la habari la Reuters.

Kansela wa Ujerumani Scholz alisema kuwa kutekeleza ukomo wa bei ni "mradi wenye matarajio makubwa na yenye mahitaji makubwa," ambao bado unahitaji "kazi kubwa."

Ingawa vikwazo vimepunguza kiasi cha mauzo ya nje ya Urusi, mapato ya Urusi yalipanda mwezi Mei, kulingana na Shirika la Nishati la Kimataifa. India na China pia zimeongeza kwa kiasi kikubwa ununuzi wao wa mafuta ghafi ya Urusi tangu vita vilipoanza, na kuipa Moscow chanzo mbadala cha mapato na uwezekano wa kutatiza mpango wowote wa bei ya ukomo.

Soma pia: Biden: Lazima tusimame pamoja dhidi ya Urusi

Rais wa Ufaransa Macron alisema Jumanne kwamba anaunga mkono kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya Urusi, na kwamba mazungumzo ya jinsi ya utekelezaji wa kiufundi yataanza hivi karibuni. Aliongeza kuwa muungano mpana zaidi utahitajika ili kufanya ukomo huo ufanye kazi.

G7 yapanga kuepusha janga la njaa

Wakati vita vya Ukraine vimesimamisha mauzo ya nafaka duniani, na kutishia mzozo wa njaa, Scholz alisema Jumanne kwamba viongozi wa G7 waliahidi dola bilioni 4.5 (€ 4.2 bilioni) ili kuimarisha upatikanaji wa chakula duniani.

Huku bandari za Ukraine zikiwa zimezuiliwa, ngano, mafuta ya alizeti, mahindi  vimekosekana kwenye soko la kimataifa, na hivyo kuongeza bei ya jumla ya vyakula. Wataalamu na mashirika ya misaada wameonya baadhi ya maeneo ya Afrika yanaweza kukumbwa na njaa hivi karibuni huku vyakula vikiisha.

Afisa wa Marekani alisema mpango huo unahusisha "juhudi za msaada katika zaidi ya nchi 47" ili "kusaidia kuokoa maisha kupitia uingiliaji wa moja kwa moja wa kibinadamu" na "kuimarisha ustahimilivu na tija ya mifumo ya chakula ulimwenguni kote, haswa katika maeneo hatarishi."

Soma pia: G7 yaweka hazina ya miundombinu kwa nchi zinazostawi

Kansela Scholz alisema Ujerumani "itahusika kwa kiasi kikubwa" katika kutoa msaada wa chakula kwa nchi zinazohitaji.

 "Wiki chache zijazo zitakuwa muhimu," alisema Rais wa Ufaransa Macron kuhusu hali ya mazao nchini Ukraine, akiongeza kuwa hifadhi zinahitajika kutolewa kabla ya mavuno ya mwaka huu.

Ujerumani yataka 'klabu ya kimataifa ya tabianchi'

Kansela wa Ujerumani Scholz pia ameshinikiza kuundwa kwa kile kinachoitwa klabu ya tabianchi, ambapo nchi ambazo zinakubaliana juu ya malengo ya hali ya hewa husamehewa ushuru.

"Tunahitaji matamanio zaidi kufikia malengo yetu ya hali ya hewa," Scholz alisema katika taarifa yake ya kufunga.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Ujerumani Jumatatu, ambayo ilijumuisha mataifa matano waalikwa yanayoendelea kama India na Afrika Kusini, viongozi walisisitiza "mabadiliko safi na ya haki ya nishati" ambayo yanapunguza matumizi ya mafuta bila kuzidisha ukosefu wa ajira.

"Ulinzi wa hali ya hewa unaweza kuwa faida ya ushindani na sio kikwazo," Scholz alisema.

Vyanzo: Reuters, dpa, AFP, AP