1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"

27 Juni 2022

Viongozi wa kundi la mataifa tajiri na ya kidemokrasia la G7 wameitumia siku ya pili ya mkutano wao wa kilele kujadili njia za kuisaidia Ukraine bila kuchoka huku wakigusia pia suala la mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/4DJoc
G7 Gipfel Schalte mit Selenskyj
Viongozi wa kundi la G7 na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya wakiwa kwenye mkutano kusini mwa Ujerumani.Picha: Tobias Schwarz/AFP

Viongozi hao wa kundi hilo linaloyajumuisha mataifa ya Ujerumani, Uingereza, Marekani, Ufaransa, Japan, Canada na Italia wameahidi leo Jumatatu kuendelea kuisdaidia Ukraine bila kuchoka katika vita vyake dhidi ya Urusi ikiwemo kuiwekea vikwazo zaidi Moscow na kuipatia mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga Ukraine.

Katika siku ya pili ya mkutano huo unaofanyika tangu jana kwenye eneo la fahari la Schloss Elmau kusini mwa Ujerumani wamesema wataendelea kuiwekea vikwazo Urusi kadri inavyohitajika na kuzidisha shinikizo la kimataifa la kiuchumi na kisiasa kwa serikali ya rais Vladimir Putin na mshirika wake mkuu, Belarus.

Kwa upande wake Marekani imesema inakamilisha awamu nyingine ya msaada wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine na sasa itapeleka mfumo wa kisasa wa ulinzi wa anga ambao rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameuomba mahsusi alipozungumza kwa njia ya video na viongozi wa G7 hapo jana.

Scholz asema vita ya Ukraine kuendelea kuwa jambo la kipaumbele kwa mataifa ya magharibi

Deutschland I G7-Gipfel auf Schloss Elmau in Garmisch-Partenkirchen
Viongozi wa G7 wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa mkutano wa kilele unaofanyika kusini mwa Ujerumani Picha: Ludovic Marin/REUTERS

Mataifa ya G7 pia yameahidi kuongeza mbinyo dhidi ya Urusi kwa kuidhibiti mifumo yake ya kifedha kupitia vikwazo na kuilenga sekta yake ya nishati kwa kujaribu kuweka ukomo wa bei ya mafuta ya Urusi kwenye soko la dunia.

Mwenyeji wa mkutano huo kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kuwa suala la Ukraine litaendelea kuwa kipaumbele kwa kundi la G7.

"Tunajadili masuala yote yaliyo kwenye ajenda, hususani kuendeleza mshikamano wa kuisaidia Ukraine dhidi ya uchokozi wa Urusi na tunaelewa kuwamba sera za mataifa yetu zinafanana sana. Nadhani huu ni ujumbe mzuri, kwamba tunachukua maamuzi magumu." amesema Kansela Scholz

Njia za kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi zajadiliwa 

Suala lingine ambalo limezungumziwa na viongozi wa G7 hii leo ni mabadiliko ya tabianchi. Viongozi wamekubaliana kufanya kazi pamoja kupambana na janga hiyo bila kuteteresha usalama wa nishati.

G7 Gipfel auf Schloss Elmauin Deutschland
Viongozi wa G7 walipojumuika na viongozi wa mataifa yaliyoalikwa mkutano wa huko Bavaria kwa majadiliano kuhusu mabadiliko ya tabianchi.Picha: Stefan Rousseau/PA/empics/picture alliance

Kwenye ajenda hiyo majadiliano yaliwajumuisha pia viongozi wa mataifa ya Argentina, India, Indonesia, Senegal na Afrika Kusini walioalikwa kuhudhuria mkutano wa G7.

Pamoja na mambo mengine wamejadili njia za kuachana na matumizi ya makaa ya mawe na kutanua uzalishaji nishati kwa kutumia vyanzo rafiki kwa mazingira.

Mzozo wa Urusi na Ukraine ambao umepandisha gharama za nishati ulimwengu unatishia kurejesha nyuma ahadi za kuachana na nishati chafuzi na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Wakati viongozi wakijadili suala hilo  kulikuwa na kundi la waandamanaji waliojaribu kufanya kila njia kupaza sauti.

Kundi la waandamanaji 50 liliruhusiwa kufanya maandamano umbali wa mita 500 kutoka ukumbi wa mikutano kuwataka viongozi hao kutangaza hatua mahsusi kukabiliana na mabadili ya tabianchi.

Mkutano huo wa G7 utakaohitimishwa kesho unayaweka mezani pia masuala ya biashara duniani, msaada zaidi kwa bara la Afrika, usalama wa chakula na mfumuko wa bei.