1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani kuiadhibu serikali yao kupitia uchaguzi wa Ulaya

4 Juni 2024

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya unafanyika wiki ijayo, lakini utafiti mpya unaonesha nchini Ujerumani mtu mmoja kwa kila watu wanne hatakwenda kupiga kura yake, kwani watu hao wanataka kuiadhibu serikali kuu ya shirikisho.

https://p.dw.com/p/4gc2X
Karatasi ya kura yenye nesmbo ya Umoja wa Ulaya ikiwekwa katika kisanduku
Bahasha yenye nesmbo ya Umoja wa Ulaya ikiwekwa katika kisandukuPicha: Panama Pictures/imago images

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya ni wa pili kwa ukubwa baada ya ule wa India. Raia wapatao milioni 450 wa Umoja wa Ulaya wanapiga kura zao kutoka tarehe 6 hadi 9 Juni.

Ujerumani ina wabunge 76 kati ya 720 wanaoshiriki kwenye bunge hilo la Strassbourg. 

Kwa wiki kadhaa sasa, wapiga kampeni wamekuwa wakiendesha harakati za kuwashawishi wapigakura, ambao wengi wao wameonesha kukosa hamu ya kushiriki uchaguzi wenyewe.

Utafiti uliofanywa na kituo cha televisheni cha ARD unaoenesha kuwa katika kila wapigakura kumi, wanne hawana mpango wa kupiga kura zao ifikapo tarehe 9 Juni.

Soma pia:Ulaya na Marekani zasusia kutoa heshima kwa Raisi

Utafiti huo uliwashirikisha wapigakura 1,515 wenye umri wa kuanzia miaka 16 kati ya tarehe 27 na 29 Mei.

Watafiti walilinganisha matokeo hayo na yale ya uchaguzi wa mwaka 2019, ambapo nchini Ujerumani waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 61, huku ule wa mwaka 2021 wakijitokeza asilimia 76.

CDU na CSU kuibuka na ushindi?

Kwa mujibu wa maoni ya wapiga kura, vyama ndugu vya CDU na CSU vina nafasi nzuri zaidi ya kuibuka kwenye nafasi za juu katika uchaguzi huo, lakini vyama vitatu vinavyounda serikali ya mseto ya Ujerumani, SPD cha Kansela Olaf Scholz, waliberali mamboleo wa FDP na walinda mazingira wa Kijani, vinaelekea kusalia mkiani.

Mfano wa karatasi ya kura katika Bunge la Ulaya
Mfano wa karatasi ya kura katika Bunge la UlayaPicha: teamwork/imago images

Chama cha Kijani ndicho hasa kinachotazamiwa kubakia chini ya asilimia 20 ya kura walizopata kwenye uchaguzi wa 2019.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, kinatazamiwa kufanya vizuri zaidi kuliko miaka mitano iliyopita, lakini asilimia 14 wanazotarajia kuzipata ni chini ya walichokuwa wakikitaka. 

Soma pia:Vyama ndugu vya kihafidhina, Christian Social Union CSU, na Christian Democratic Union nchini Ujerumani vyashinda katika chaguzi za kijimbo

Muungano wa Sahra Wagenknecht, kundi lililojienguwa kutoka chama cha mrengo wa kushoto, die Linke, miezi michache iliyopita, unatazamiwa kuibuka na asilimia sita tu, lakini hata kiwango hicho ni kikubwa sana mbele ya die Linke, Free Voters na FDP.

Hata hivyo, nusu ya walioshiriki kwenye utafiti huo walisema walishaamua wa kumpigia kura.

Masuala muhimu wanayozingatia wapiga kura

Walipoulizwa masuala ambayo wameyaangalia kwenye kuamua wa kumpigia kura, walisema ni masuala ya amani, usalama wa kijamii na uhamiaji.

Masuala haya ni tafauti na yale ya miaka mitano iliyopita, ambapo mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa mazingira yalikuwa ndivyo vipaumbele vya wapigakura wa Ujerumani.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

Mwaka 2019, wapiga kura hao walikuwa wanauangalia Umoja wa Ulaya kwa jicho zuri zaidi kuliko sasa, ambapo ni wanne tu kati ya kumi waliosema kuwa wanaamini uanachama kwenye Umoja huo kuna faida zaidi kwa Ujerumani.

Soma pia:Macron na Scholz wazungumzia mzozo wa Ukraine

Kwa asilimia 19, hasara za Umoja wa Ulaya ni nyingi kuliko faida zake. Miaka mitano iliyopita, asilimia 55 ya wapigakura walipendelea wazo la kuhamishia madaraka ya serikali kwenye Umoja wa Ulaya, lakini sasa idadi hiyo imechuka hadi asilimia 48.

Wapigakura wengi wana mtazamo hasi, huku wafuasi wa BSW na AfD kwa ujumla wakiwa na mashaka au hata kabisa wakiuchukia Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo, nusu ya wafuasi wa SPD, Kijani, CDU na CSU walielezea wasiwasi wao juu ya mustakabali wa Umoja huo.

Huu ni uchaguzi ambao rais wa sasa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ambaye ni Mjerumani na mwanachama wa +CDU, anaomba tena kuchaguliwa kwenye wadhifa huo, lakini ajabu ni kuwa ni wapigakura wanne tu katika kila kumi ndio wanamuunga mkono - wengi wao wakiwa wafuasi wa CDU, CSU, SPD na walinda mazingira wa Kijani.