1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Scholz wazungumzia mzozo wa Ukraine

29 Mei 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamezungumzia umuhimu wa Umoja wa Ulaya na ushirikiano katika masuala ya uvumbuzi, uchumi na mikakati ya ulinzi.

https://p.dw.com/p/4gPdu
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kushoto, na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kushoto, na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wakisalimiana katika kasri la Meseberg 28.05.2024Picha: Filip Singer/EPA

Suala kubwa ambalo lilitawala mazungumzo kati ya Scholz na Macron ni vita vinavyoendekea nchini Ukraine. Scholz alisema wanataka kuendelea kuisadia Ukraine kisiasa, kifedha, kijeshi na kwa kuipa misaada ya kibinadamu.

Alisema Uhispania tayari imeshaahidi kutoa msaada na kwamba yeye na Macron wamekubaliana ni lazima wachukue hatua inayofuata kuimarisha msaada huu katika ngazi nyingine mpya.

Scholz alisema wanataka kuisaidia Ukraine ipate mabilioni ya fedha kama msaada zaidi ili iweze kukidhi mahitaji yake ya ulinzi na hivyo kuimarisha usalama wa Ulaya.

 "Kipaumbele chetu kikuu kinabaki kuisaidia Ukraine kwa uwezo wetu mzuri kabisa kadri tunavyoweza. Hii inahusu hasa upelekeji wa mifumo ya ulinzi wa anga na kuijenga upya miundombinu ya nishati iliyoharibiwa vibaya."

"Tumeahidi tutaisaidia Ukraine kwa kipindi kirefu kadri itakavyohitajika. Kama washirika, sote, Ujerumani na Ufaransa, Marekani, Uingereza, Japan, Canada na Ulaya kwa ujumla na washirika wengine wengi, tumekuwa tukitoa msaada mkubwa kwa zaidi ya miaka miwili," aliongeza kusema Scholz.

Macron ataka Ukraine iruhusiwe kuziharibu kambi za Urusi

Kwa upande wake rais Macron alisema anapanga kuwasilisha mpango katika wiki zijazo kuhusu uwezekano wa kupeleka wakufunzi wa jeshi la Ufaransa kwenda Ukraine, wakati serikali ya mjini Kiev ikijizatiti kuyazuia mashambulizi ya Urusi.

Lettland | Wolodymyr Selenskyj in Riga
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Gints Ivuskans/AFP

Macron anapanga kufanya hivyo wakati wa ziara ya rais wa Ukraine Volodymry Zelensky huko Normandy kwa kumbukumbuku ya kutua kwa majeshi ya muungano katika pwani ya Normandy wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.

"Msaada wetu kwa Ukraine utaendelea kadri utakavyohitajika. Tumeimarisha kwa pamoja utoaji misaada katika mieizi michache iliyopita. Kando na Ukraine bila shaka ni suala la kuimarisha usalama wetu, ulinzi wa pamoja barani Ulaya na miongoni mwa Wazungu, jambo ambalo limetukaa mioyoni mwetu," alisema Macron.

Rais Macron  pia alisema Ukraine inatakiwa iruhusiwe kuzishambulia na kuziharibu kambi za jeshi la Urusi zinazotumiwa kufyetulia makombora katika ardhi ya Ukraine.

Scholz na Macron pia waligusia hali inayoendelea katika Ukanda wa Gaza na nchini Israel.

Soma pia: Macron aendelea na ziara ya siku tatu nchini Ujerumani

Wakati haya yakiarifiwa, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell, amesesma nchi za Ulaya bado zimegawika kuhusu kuwapeleka wakufunzi wa kijeshi Ukraine. Nchi za Ulaya zimewapa mafunzo wanajeshi 50,000 wa Ukraine nje ya nchi hiyo inayokabiliwa na vita chini ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya ulioanzishwa mwaka 2022.

Katika uwanja wa mapambano Ukraine inasema watu saba wameuliwa katika maeneo manne huku Urusi ikiendelea kuyadhibiti maeneo katika uwanja wa vita ambako wanajeshi wa Ukraine wanapata changamoto. Maafisa wa Ukraine wamesema shambulizi la kombora hivi leo katika eneo la Sumy linalopakana na Urusi limewaua watu wawili na kuwajeruhi wengine watatu.

(afpe, dpa)