1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Utafiti: Watu 1,329 wafa kutokana na njaa huko Tigray

26 Septemba 2023

Utafiti uliofanywa na mamlaka za afya na Chuo Kikuu cha Mekele katika jimbo la Tigray umebaini kuwa njaa ndio sababu kuu ya vifo katika mkoa huo uliopo kaskazini mwa Ethiopia.

https://p.dw.com/p/4Woso
Äthiopien | Tigray Krise Nahrungsmangel
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Utafiti huo unatokana na sensa ya kaya iliyofanywa na wahudumu wa afya kuanzia Agosti 15 hadi 29 katika vitongoji tisa vya Tigray na kambi 53 za wakimbizi wa ndani. Mkoa wa Tigray kwa jumla una vitongoji 88 na kambi 643 za watu waliolazimika kuyahama makazi yao. 

Soma pia: Mgogoro wa Ethiopia watishia uthabiti wa kikanda-UN

Sababu mojawapo ya kutokea maafa hayo ya njaa ni kusitishwa kwa msaada wa chakula kutoka Marekani na Umoja wa Mataifa baada ya kugunduliwa mnamo mwezi Machi wizi mkubwa wa nafaka katika eneo hilo la Tigray.

Usitishaji huo uliwekwa kwa nchi nzima ya Ethiopia mnamo mwezi Juni baada ya kugundulika kuwa wizi huo ulienea kwenye nchi nzima.

Chakula cha msaada kutoka Marekani kwa watu wa Ethiopia
Chakula cha msaada kutoka Marekani kwa watu wa EthiopiaPicha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Ethiopia inataka vikwazo hivyo viondolewe mara moja huku Marekani na Umoja wa Mataifa nazo zinaitaka serikali ya Ethiopia iache kudhibiti mfumo wa utoaji misaada ya chakula.

Huku mivutano ikiendelea kati ya serikali ya Ethiopia na wafadhili wakuu, idadi ya vifo kutokana na sababu zilizoorodheshwa na watafiti katika maeneo mbalimbali kwenye mkoa wa Tigray imeongezeka.

Soma pia: Marekani yasimamisha misaada ya chakula nchini Ethiopia

Maeneo yaliyofanyiwa utafiti yamebainika kwamba idadi hiyo ya watu wanaokufa kwa njaa imeongozeka kwa karibu mara mbili hasa baada ya kusitishwa misaada kuanzia watu 159 mnamo mwezi Machi hadi watu 305 katika mwezi wa Julai.

Takriban watu milioni 5.4 kati ya wakazi milioni 6 wa Tigray wanategemea misaada ya chakula. Zaidi ya watu milioni 20 nchini Ethiopia kwa ujumla wanahitaji msaada wa chakula.

Watu wa Tigray wakipokea msaada wa chakula
Watu wa Tigray wakipokea msaada wa chakulaPicha: Eduardo Soteras/AFP

Matokeo ya utafiti huo yameandaliwa na Kituo cha Uratibu wa Dharura cha Tigray, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya misaaada na ofisi ya serikali ya kikanda. Taarifa hiyo pia imethibitihswa na shirika la Habari la Associated Press.

Soma pia: Shirika la WFP larejesha msaada wa chakula Ethiopia

Kuhusiana na swala wa wizi wa nafaka, mapema mwezi huu, kiongozi wa eneo la Tigray alitangaza kuwa maafisa 480 walikamatwa kuhusiana na ufisadi huo. Sehemu zingine nchini Ethiopia bado hazijatangaza matokeo ya uchunguzi wao.

Marekani na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa WFP pia zimesema bado zinaendelea na uchunguzi. 

Chanzo:AP