1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Ubaguzi dhidi ya watu weusi bado upo Ulaya

25 Oktoba 2023

Utafiti uliofanywa na Shirika la Ulaya la Haki za Msingi (FRA), juu ya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi katika Mataifa 13 ya Umoja wa Ulaya, umeitaja Ujerumani kuongoza ikilinganishwa na maeneo mengine.

https://p.dw.com/p/4Y0kQ
Waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi mjini Berlin, Ujerumani
Waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi mjini Berlin, UjerumaniPicha: Christian Mang/REUTERS

Kwa mujibu wa utafiti huo takriban asilimia 77 ya waliohojiwa nchini Ujerumani walisema wamewahi kubaguliwa katika miaka mitano iliyopita kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, asili yao au dini yao.

Idadi hii ikitajwa kuwa kubwa zaidi kati ya nchi 13 za Umoja Ulaya ambazo watu wenye asili ya Kiafrika walihojiwa kuhusu ubaguzi wa rangi.

Huku Austria, ambako ni makao makuu ya shirika la Ulaya la Haki za Msingi (FRA), iliorodheshwa pia kuwa na kiwango cha juu cha ubaguzi wa rangi.

Takribanasilimia 45 ya zaidi ya washiriki 6,700 wa utafiti huo barani Ulaya walipitia ubaguzi wa kikabila katika miaka ya hivi karibuni. Takwimu ambazo ni asilimia sita zaidi ya utafiti uliofanywa mwaka 2016.

Soma pia:Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ubaguzi wa Rangi (CERD) yaelezea wasiwasi kuhusu soka ya Italia

Kulingana na utafiti huo, Ujerumani pia iko juu ya orodha kwa matukio ya mashambulio yaliyochochewa na ubaguzi wa rangi, huku asilimia 54 ya waliohojiwa wakisema walinyanyaswa, ambayo vile vile ni asilimia ya juu zaidi kati ya mataifa 13 yaliyoshiriki katika utafiti huo.

Aidha asilimia 9 ya waliohojiwa waliripoti kwamba jamaa zao walipitia unyanyasaji nchini Ujerumani.

Hata hivyo katika matukio ya namna hii Finland iliizidi Ujerumani na imeorodheswa kuwa na asilimia 11.

Wanafunzi wakabiliwa na ubaguzi zaidi Ujerumani

Zaidi ya nusu ya watu weusi waliohojiwa nchini Ujerumani walihisi kubaguliwa wakati wa kutafuta ajira. 

Wanafunzi wakielekea shule Ujerumani
Wanafunzi wakielekea shule UjerumaniPicha: Abdulhamid Hosbas/Anadolu Agency/picture alliance

Utafiti wa shirika la FRA vile vile umebainisha kwamba karibu asilimia 40 ya wanafunzi weusikatika shule za Ujerumani wanakabiliwa na matusi au vitisho vya ubaguzi wa rangi, sawa na Ireland, Finland na Austria.

Soma pia:Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi kufanyika Ufaransa

Mkurugenzi wa shirika la FRA Michael O'Flaherty ameitaja hali hiyo kama "ya kushtusha " na kuongezea kwamba Umoja wa Ulaya na nchi wanachama lazima wakuze juhudi zao na kuhakikisha watu wa asili ya Kiafrika wanaweza kufurahia haki zao kwa uhuru bila ubaguzi wa rangi."

Aidha shirika hilo limetoa wito kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya kukusanya data sahihi zaidi kuhusu matukio ya ubaguzi wa rangi na kutoa adhabu kali zaidi kwa uhalifu wa kibaguzi.