1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yashambulia mji alikokulia Rais Zelensky

19 Mei 2023

Urusi imefanya wimbi la mashambulizi ya angani Ijumaa yaliyosababisha moto kwenye majengo kadhaa katika mji wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

https://p.dw.com/p/4RZMV
Picha ya maktaba inayoonyesha jengo lililoharibiwa wakati Urusi iliposhambulia mji wa Kryvyi Rih Disemba 16, 2022.
Picha ya maktaba inayoonyesha jengo lililoharibiwa wakati Urusi iliposhambulia mji wa Kryvyi Rih Disemba 16, 2022.Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Kufuatia mashambulizi makali ya angani yaliyofanywa na vikosi vya Urusi mapema leo dhidi ya mji ulioko eneo la kati la Ukraine Kryvyi Rih, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 64 amejeruhiwa vibaya.

Kulingana na taarifa ya ikulu ya rais mjini Kiev, vikosi vya Urusi vilishambulia kiwanda binafsi, na majengo kadhaa yakashika moto kwa wakati mmoja.

Mjini Kiev, ving'ora vya tahadhari vilisikika kila upande na maeneo mengi ya nchi usiku wa kuamkia leo, huku mifumo ya ulinzi ikitafuta ndege zisizo na rubani zinazotumiwa kufanya mashambulizi.

Urusi yaifyatulia Ukraine makombora 30

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar amesema leo kwamba vikosi vya Urusi vinajaribu kukamata maeneo ambayo wamepoteza karibu na mji wa mashariki Bakhmut, lakini vikosi vya Ukraine vinazuia mashambulizi yao.

Maliar amethibitisha kuwa vikosi vya Urusi vimekamata sehemu za mji huo lakini hawana udhibiti na mapigano yanaendelea. 

Ukraine: Tumevirejesha nyuma vikosi vya Urusi huko Bakhmut

Tangu mwezi uliopita, Urusi imeimarisha kampeni yake ya kufanya mashambulizi ya masafa marefu hususan wakati wa usiku.

Ukraine yahusisha operesheni ya Urusi na wasiwasi wa mashambulizi ya kukomboa maeneo ya nchi

Mji wa Bakhmut umeharibiwa pakubwa kufuatia mapigano ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa.
Mji wa Bakhmut umeharibiwa pakubwa kufuatia mapigano ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa.Picha: Libkos/AP Photo

Jeshi la Ukraine limesema liliangusha makombora 16 kati ya 22 yaliyofyatuliwa. Takwimu hiyo inaonyesha hali isiyo ya kawaida ya idadi kubwa yaa makombora ya Urusi ambayo hayakuangushwa.

Maafisa wa Ukraine hawakutoa maelezo zaidi kuhusu maeneo mengine yaliyoshambuliwa isipokuwa mji wa Kryvyi Rih unaozalisha chuma na vilevile ndio mji alikokulia rais Volodymyr Zelensky.

Ukraine yashutumu Urusi kwa kufanya mashambulizi mabaya

Ukraine inahusisha ongezeko la mashambulizi ya angani dhidi yake kama wasiwasi wa Urusi kuhusu mashambulizi yanayotarajiwa ya Ukraine yanayolenga kurejesha mikononi mwake, maeneo ambayo Urusi imenyakua kusini na mashariki mwa nchi hiyo.

Mwanzilishi wa kampuni binafsi ya wapiganaji ya Urusi Wagner Yevgeny Prigozhin naye amesema leo Ijumaa kwamba haiwezekani kwa mji huo kuwa kwenye udhibiti wao kabisa katika muda wa siku mbili zijazo, kutokana na ngome ya ulinzi wa wanajeshi wa Ukraine wanaopigana nao mjini humo.

Mji huo umeharibiwa pakubwa kutokana na vita ambavyo vimedumu kwa miezi kadhaa sasa.

Na kule Zaporizhzhia, mashuhuda wanne wamesema katika majuma ya hivi karibuni, vikosi vya Urusi vimekuwa vikijiimarisha karibu na mtambo wa nishati ya nyuklia, kuelekea makabiliano yanayotarajiwa jimbo hilo. Wameongeza kusema kuwa mahandaki mapya yamechimbwa mjini humo na mabomu zaidi yametegwa

(VYANZO: RTRE, AFPE)