1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaishambulia Kyiv

29 Julai 2022

Jeshi la Urusi limevishutumu vikosi vya Kyiv kwa kuishambulia jela inayowashikilia wafungwa wa vita wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Eqr0
Ukraine Krieg, Angriff auf Mykolaiv
Picha: Press service of the State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Katika eneo linalodhibitiwa na waasi mashariki mwa Ukraine, likisema watu 40 wameuwawa na wengine wengi kujeruhiwa. 

Wizara ya ulinzi ya Urusi katika taarifa yake imethibitisha kuuwawa kwa wafungwa 40 wa kivita wa Ukraine na kuwajeruhi wengine 75, na kuongeza kuwa wafanyakazi wanane wa jela hiyo iliyoko Olenivka eneo linalodhibitiwa na waasi wanaotaka kujitenga la Donetsk pia walijeruhiwa.

Huku haya yakijiri kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa, wanajeshi wa Urusi wamefanya mashambulizi ya roketi kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

soma Zelensky: Tutapata Ushindi dhidi ya uvamizi wa Urusi

Kulingana na gavana wa mkoa wa Kyiv, Oleksiy Kuleba, watu 15 wamejeruhiwa na mashambulizi hayo yalilenga vituo vya kijeshi kwenye viunga vya mji wa Kyiv.

Gavana Kuleba aliiambia televisheni ya taifa kwamba makombora zaidi ya Urusi pia yalianguka katika mji wa Chernihiv ulioko kaskazini mashariki mwa mji mkuu.

soma Mashambulizi yaliyoilenga bandari ya Odessa yalaaniwa

Mashambulizi ya Urusi katika mji wa Mykolaiv wa Ukraine ulioshambuliwa kwa mabomu karibu na mstari wa mbele wa kusini mwa nchi hiyo yaliwauwa watu watano katika kituo cha basi na kuwajeruhi wengine saba.

Ofisi ya rais wa Ukraine, Voloydmir Zelensky, leo Ijumaa imesema kwamba makombora ya Urusi yaliyoipiga Mykolaiv yaliharibu majengo kadhaa, pamoja na nyumba za makazi.

Marekani yasema Urusi imetoa vitisho vipya

Antony Blinken
Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema Urusi imetoa "vitisha vipya"kwamba inatazamia kuchukua kimabavu maeneo zaidi ya Ukraine mbali na Donbas, akiongeza kuwa hatua kama hiyo "haitahalalishwa kamwe."

Akizungumza na waandishi wa habari Blinken amesema "Nadhani ni muhimu sana sasa tuone nini mpango unaofuata wa Urusi: huo ni unyakuzi wa eneo zaidi la Ukraine. Waziri wa Mambo ya nje Lavrov atasikia moja kwa moja kutoka kwangu kwa niaba ya Marekani, tunaona na tunajua wanachofanya na hatutakubali kamwe, haitahalalishwa kamwe, kutakuwa na matokeo ikiwa ndivyo wanavyofanya, na ikiwa ndivyo wanavyojaribu kudumisha"

Haya yanajiri wakati Marekani ilitangaza hapo jana kuwa imewasilisha pendekezo kwa Moscow la kuachiwa huru Wamarekani wawili wanaoshikiliwa nchini Urusi akiwemo mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu nchini Marekani, Brittney Griner.

Waziri wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov amesema Moscow hivi karibuni itapendekeza siku ya mazungumzo hayo na Marekani.