1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky anaamini watapata ushindi dhidi ya Urusi

28 Julai 2022

Wakati akisherehekea sikukuu mpya ya kuashiria utaifa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema leo kuwa ana uhakika wa kupata ushindi dhidi ya uvamizi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4ElRC
Ukraine Rede Präsident Selenskyj
Picha: Alexey Furman/Getty Images

Katika Siku hiyo ya kwanza ya Kitaifa ambayo itakuwa ikiadhimishwa sambamba na Siku ya Uhuru Agosti 24, Rais Zelensky amewapongeza raia wa Ukraine kwa ushupavu na ukakamavu wao, na kusema ilikuwa asubuhi ya taabu iliyogubikwa na makombora, lakini raia wa Ukraine hawakukata tamaa.

Zelensky amechapisha video yenye hisia kuhusu mapambano yanayoendelea na kusisitiza kuwa Ukraine ni nchi huru na isiyogawanyika. Na itakuwa hivyo milele na kuendelea kupigania uhuru wake. Hapo awali, kiongozi anayeiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine na anayetaka kujitenga Denis Pushilin amesema wakati umewadia wa kuidhibiti miji ya Kharkiv, Odessa na hata Kyiv.

Soma zaidi: Urusi yatoa hakikisho la usafirishaji wa ngano

Hayo yanajiri wakati Vikosi vya Urusi vimeanzisha leo mashambulizi makali ya makombora kuelekea mikoa ya Kyiv na Chernihiv, maeneo ambayo yalikuwa hayajashambuliwa kwa wiki kadhaa, huku maafisa wa Ukraine wakitangaza operesheni ya kukomboa eneo lililokaliwa kwa mabavu kusini mwa nchi hiyo.

Gavana wa mkoa wa Kyiv Oleksiy Kuleba na yule wa Chernihiv Vyacheslav Chaus wamethibitisha mashambulizi hayo ya makombora lakini hadi sasa haijafahamika idadi ya walioathirika.

Ukraine-Konflikt, von Artillerie beschädigte Brücke in Cherson
Picha: Sergei Bobylev/ITAR-TASS/IMAGO

Operesheni ya Jeshi la Ukraine

Jeshi la Ukraine limeendelea kushambulia eneo la kusini linalokaliwa la Kherson, ambapo siku ya Jumatano lilifaanikiwa kushambulia na kubomoa daraja muhimu linalotumiwa na Urusi katika mto Dnieper.

Maafisa waliowekwa na Urusi eneo hilo la kusini mwa Ukraine wamesema leo kuwa zaidi ya "wasaidizi" 20 wa jeshi la Ukraine na idara za usalama wamezuiliwa huku silaha mbalimbali zikiwemo mabomu 53 ya kurushwa kwa mkono na zaidi ya kilo 24 za vilipuzi vikikamatwa.

Soma zaidi: Serikali za Umoja wa Ulaya zakubaliana kuhusu mgawo wa gesi asilia

Jana, Urusi ilipunguza mtiririko wa gesi kuelekea barani Ulaya katika mvutano wa nishati na Umoja wa Ulaya. Imezuia pia usafirishaji nje ya nchi wa nafaka za Ukraine tangu ilipoivamia, Ijumaa iliyopita, walikubali kuruhusu tena usafirishaji kupitia Bahari Nyeusi hadi nchini Uturuki kuelekea kwenye masoko ya kimataifa. Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar amesema maandalizi yanaendelea vyema:

"Kituo cha uratibu kinaweza kufuatilia mienendo ya meli zote za wafanyabiashara katika Bahari Nyeusi kwa kutumia miundombinu ya Uturuki. Maandalizi na mipango ya meli ya kwanza iliyosheheni nafaka na itakayo ondoka bandari ya Ukraine bado inaendelea."

Soma zaidi: Urusi yasema mashambulizi bandari ya Odessa yalilenga silaha za Marakeni

Makubaliano hayo yalitiwa dosari na kuzuka hofu ya kuvunjika wakati Urusi ilipoishambulia kwa makombora bandari kubwa nchini Ukraine ya Odesa, siku moja tu baada ya kusainiwa mkataba huo wa nafaka.Kabla ya uvamizi na vikwazo vilivyofuata, Urusi na Ukraine ilichangia karibu theluthi moja ya mauzo ya nje ya ngano duniani kote.

(DPAE, AP, AFP, RTRE)