Mashambulizi yaliyoilenga bandari ya Odessa yalaaniwa
24 Julai 2022Mashambulizi hayo kwenye bandari hiyo ya Bahari Nyeusi yamezusha ukosoaji mkubwa kutoka ndani ya Ukraine na upande wa magharibi. Ukraine imesema chini ya mkataba uliosainiwa mjini Instabul, mashambulizi ya aina hiyo yamezuiwa.
"Hapo jana (Ijumaa) usafirishaji wa kutumia bahari uliafikiwa, na hii leo (Jumamosi) Urusi wanaishambulia bandari ya Odessa," alisema mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, Andree Yermak alipozungumza muda mfupi baada ya kutokea mashambulizi.
Kulingana na jeshi la Ukraine, makombora mawili ya Urusi yalidunguliwa na mifumo ya ulinzi lakini mengine mawili yaliipiga bandari hiyo ya kibiashara. Duru zinasema watu kadhaa walijeruhiwa lakini hakuna ghala la nafaka lililoharibiwa.
Ukraine imelaani shambulizi hilo ikilitaja kuwa dharau kwa Uturuki na Umoja wa Mataifa zilizofanya kazi ya kutafuta mkataba wa kuruhusu kusafirishwa nafaka.
Marekani yasema Urusi inahujumu mkataba wa Istanbul
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema shambulizi hilo linadhoofisha kazi iliyofanywa na Umoja wa Mataifa, Uturuki na Ukraine ya kuwezesha kupatikana mkataba wa upelekwaji wa chakula katika masoko ulimwenguni.
Blinken amesema hujuma hiyo "imezusha mashaka" juu ya dhamira ya Moscow kwenye kutekeleza mkataba wa kuruhusu kusafirishwa kwa nafaka ya Ukraine iliyokwama.
Kwenye mkataba uliotiwa saini mnamo siku ya Ijumaa, Urusi iliahidi kuruhusu meli kupita bila kizuizi katika ujia wa Bahari Nyeusi na haitozishambulia. Bandari zilizopo kwenye eneo hilo la mwambao hazitoshambuliwa.
Ukraine yasema Urusi itawajibika iwapo makubaliano yatavunjika
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameituhumu Urusi kwa kukiuka makubaliano hayo. "Chochote ambacho Urusu huahidi, basi hutafuta njia ya kukitimiza," alisema Zelensky.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Ukraine Oleg Nikolenko ameyafananisha mashambulizi hayo kuwa sawa na rais Vladimir Putin wa Urusi "kuwatemea mate usoni" Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Guterres alilaani kwa nguvu zote mashambulizi hayo huku msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq akisema utekelezaji wa makubaliano hayo ni muhimu ili kutatua mgogoro wa upungufu wa chakula duniani na kupunguza mateso ya mamilioni ya watu.
Ukraine imesema kinagaubaga kuwa Urusi itabeba dhima kwa mzozo wowote wa chakula ikiwa makubaliano yaliyosainiwa yatavunjika.