1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani kuwasilisha rufaa dhidi ya ushindi wa Museveni

18 Januari 2021

Chama cha upinzani Uganda cha NUP kinajiandaa kuwasilisha rufaa mahakamani kupinga kutangazwa kwa Yoweri Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Alhamisi iliyopita, huku kiongozi wa chama hicho Robert Kyagulanyi akiwa chini ya kizuizi cha nyumbani kisicho rasmi.

https://p.dw.com/p/3o4HW

Baada ya mgombea Yoweri Museveni Tibuhaburwa kupata kura za juu zaidi katika uchaguzi na kwa kuwa kura alizopigiwa ni zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, tume ya uchaguzi ilimtangaza Yoweri Museveni Tiburhaburwa kuwa rais aliyechaguliwa wa Jamhuri ya Uganda.

Hii ni baada ya kutamka kuwa Museveni alipata asilimia 58.64 ya kura zilizohesabiwa. Kati ya wagombea 10 wengine, mshindani mkubwa alikuwa Robert Kyagulanyi ajulikanaye zaidi kama Bobi Wine ambaye alitangazwa kupata asilimia 34.83 ya kura zilizohesabiwa.

Uganda Kampala | Präsidentschaftswahl: Bobi Wine während Pressekonferenz
Bobi Wine bado yupo chini ya kifungo cha nyumbani Picha: Nicholas Bamulanzeki/AP/picture alliance

Hata hivyo, upande wa Bobi Wine umepinga matokeo hayo ukidai kuwa palitokea udanganyifu mkubwa katika kuwasilisha matokeo pamoja na kwamba wawakilishi wao kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura walifukuzwa na jeshi na polisi wakati shughuli hiyo ilipokuwa ikiendelea.

"Tunakanusha na kupinga matokeo yaliyosomwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kwa sababu si sawa na yaliyotolewa katika vituo mbalimbali vya kupigia kura nchini" amesema Benjamin Katana ni mhazini wa chama cha NUP ambaye alikuwepo kwenye kituo cha kitaifa ambapo tume ilitangaza matokeo hayo.

Serikali yasema haishangazwi na madai hayo 

Bildkombo | Yoweri Museveni und Bobi Wine
Mchuano ulikuwa mkali kati ya rais Yoweri Museveni na Bobi Wine

Hata hivyo, msemaji wa serikali Ofwono Opondo amelezea kuwa hashangazwi na kauli ya NUP kwamba hawakubaliani na matokeo hayo.

"Hakuna uchaguzi hata mmoja ambao haujawahi kupingwa na kila mara suala hilo huishia mahakamani. Lakini mahakama hizo zimeiondolea NRM na hasa rais Museveni lawama" amekaririwa Opondo.

Hadi sasa Bobi Wine amendelea kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani. Haruhusiwi kutoka wala mtu yeyote kuingia kwake.

Ila naibu msemaji wa majeshi Luteni Kanali Deo Akiiki amekanusha madai hayo akasema "kile ambacho tunampa ni usalama ambao hutolewa kwa wagombea wote. Yeye si raia wa kawaida kwa hiyo ni jukumu letu kuona kwamba kila Mganda na kila mgombea wako na usalama"

Wakati huohuo kurejeshwa kwa mawasiliano ya inteneti kumeletea nafuu watumiaji. Lakini kasi yake ingali ya chini na wakati mwingine mawasiliano hayo yanakatika.