1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Usalama wa chakulaUlaya

UN yaonya juu ya kupungua kwa uzalishaji wa nafaka Ukraine

22 Novemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limetahadharisha kuwa uzalishaji wa ngano wa Ukraine huenda ukashindwa kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4ZHuo
Mzozo wa chakula duniani
Mkulima raia wa Ukraine akionyesha nafaka za ngano katika mji wa OrikhivPicha: Oleksandr Ratushniak/REUTERS

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limetahadharisha kuwa uzalishaji wa ngano wa Ukraine huenda ukashindwa kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya taifa iwapo njia za usafirishaji kupitia bahari nyeusi zitafungwa na mashambulizi kwenye miundombinu ya chakula yataendelea.

Mkurugenzi wa WFP nchini Ukraine Matthew Hollingworth amesema ripoti ijayo ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, itaonyesha kuwa tangu katikati ya mwezi Julai, kumekuwepo na mashambulizi 31 yaliyolenga miundombinu ya chakula nchini humo.

Hollingworth ameliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa kuwa, kati ya mashambulizi hayo, 28 yalikuwa katika mkoa wa Odesa, ambao una mji na bandari muhimu kwa ajili ya biashara ya kimataifa.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia ameliambia baraza hilo la usalama jana kuwa, Moscow inalenga miundombinu ya kijeshi ya Ukraine na wala sio miundombinu ya raia.

Umoja wa Mataifa umeilaumu Urusi tangu uvamizi wake mnamo mwezi Februari mwaka jana kwa kuzidisha mzozo wa chakula duniani. Ukraine na Urusi ni wazalishaji wakubwa wa nafaka duniani.