1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukatili dhidi ya wanawake ukomeshwe

24 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CBJS

Hakuna anaeweza kubisha ukweli kuwa wanawake,wakati wa vita hujikuta katika hali ya kukhofia vitendo vya ukatili na uonevu hasa kuhusu miili yao.Lakini kuwa wanawake wakati wa amani pia wanakabiliwa na vitisho hata katika familia zao zenyewe ni hali inayoendelea kufichwa.Umoja wa Mataifa umetangaza Novemba 25 kama ni siku ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake kote duniani.

Mwezi Februari mwaka huu,msichana wa Kijerumani mwenye asili ya Kituruki,alipopigwa risasi na kuuawa barabarani mjini Berlin,watu walishtushwa sana nchini Ujerumani.Hatun Sürücü aliekuwa na miaka 23 aliuawa na kaka yake mwenyewe kwa sababu eti “alikuwa akifuata sana tabia za Kijerumani”.Hata kabla ya kutokea kifo hicho,si chini ya wanawake wanane wengine waliuawa nchini Ujerumani kwa sababu kama hizo.Wanaume katika familia zao walichukua hatua kuhifadhi heshima ya ukoo kwa vile wanawake walitaka kukimbia udhalimu na unyanyasaji katika familia zinazodhibitiwa na wanaume.Walichotaka kwa kweli wanawake hao ni kutekeleza haki zao za kujiamulia wenyewe maisha yao nchini Ujerumani.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa linalotetea haki za binadamu-Amnesty International,kote duniani,mwanamke mmoja kutoka wanawake watatu, katika maisha yake,ama hupigwa,hulazimishwa kujamiana au hudhalilishwa kwa njia zingine.

Familia na mazingira ni jamii ndogo inayopaswa kushsughulikia migogoro na kusuluhisha matatizo. Wakati huu wa utandawazi,tamaduni na thamani za kijadi hukabiliwa na changamoto mpya.Ikiwa mwanamume anaehisi hana thamani kwa sababu ya kupungukiwa hadhi na uwezo wa kiuchumi,atatumia ukatili kuonyesha nguvu zake dhidi ya mwanamke alie dhaifu kimaumbile,basi hilo si pigo tu la kurudi nyuma bali pia ni ishara ya ubabaikaji.

Tangu miaka,mtafiti wa Kijerumani,Christian Pfeiffer anaeshughulikia masuala ya uhalifu wa vijana ameonya kuwa kuna pengo kubwa kati ya ndoto za vijana wengi wa kiume na ukweli wa maisha.Katika vyombo vya habari sura ya wanaume inayotolewa ni ile ya mbabe wa michezo ya kuigiza,Rambo anaetumia nguvu kupata kile anachotaka-yeye hushangiriwa na huigizwa na vijana.Lakini ukweli wa mambo ni kuwa katika maisha ya kila siku na kazini ni mwanamume wa aina nyingine kabisa anaetakiwa-yaani mwanamume anaeweza kushirikiana na kuwasiliana na wenzake,akiwa na kipaji cha kuelewa hisia za wengine na vile vile kuwa tayari kumkubali mkuu alie mwanamke.

Lakini kijana anaekulia katika mazingira ambako kanuni za wanaume huamua maisha,baadae anapokuwa mtu mzima huona shida kubadilisha kanuni hizo.Hasa ikiwa matakwa ya kujifanya kuwa ni bora zaidi,yamepitwa na wakati kulingana na ukweli wa mambo vile yalivyo.

Kwa sababu hiyo si serikali,wanasheria na majaji tu wanaohitajiwa kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake kote duniani,bali kuna haja pia ya kuwa na watu watakaotoa mifano mizuri katika jamii.Kinachohitajiwa hasa ni wanaume zaidi wasiojaribu kudumisha hisia za utawala wa madume. Wanahitajiwa wanaume shujaa wenye uwezo wa kuonyesha hisia na kuwasiliana na wengine na wanaojiamini kuishi vingine kabisa na kuwa mfano mpya wa maisha ya wanaume.