1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaridhia masharti magumu kwa wahamiaji

7 Novemba 2023

Masharti magumu zaidi ya kuzuwia idadi kubwa ya wakimbizi kuingia Ujerumani yamefikiwa na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, katika mkutano wake na viongozi wa majimbo yote 16 yanayounda Ujerumani.

https://p.dw.com/p/4YVJa
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Mikakati hiyo mipya inajumuisha kuharakisha mchakato wa waomba hifadhi, kudhibiti gharama za wahamiaji na ongezeko la bajeti kwa serikali za majimbo kutoka kwa serikali kuu mjini Berlin, ili kushughulikia gharama za kuwapokea wahamiaji.

Akizungumza baada ya majadiliano marefu, kansela Scholz ameyaita makubaliano haya ya kihistoria, matamshi yanayoonyesha ni kwa namna gani suala hilo limekuwa tatizo kubwa kwa serikali yake.

Scholz kukutana na wakuu wa majimbo kujadili wahamiaji

Serikali ya Scholz imekubali kuyalipa majimbo na mabaraza ya Ujerumani euro 7,500 kwa kila mkimbizi mmoja kwa mwaka, kuanzia mwaka ujao na pia kufanya malipo ya mapema ya euro bilioni 1.75 ya nusu, kwa mwaka wa kwanza wa mwaka 2024. Kiongozi wa jimbo la Hesse aliweka idadi jumla ya fedha za msaada kufikia euro bilioni 3.5

Serikali hizo pia za majimbo zinatazamia kupata takriban euro bilioni moja, kwa kupunguza fedha za msaada kwa waomba hifadhi kwa kuongeza mara mbili, muda wakusubiri hadi pale watakapopata fedha kamili za usaidizi na kuingia katika mfumo wa ujerumani.

Katika mkutano huo kati ya scholz na viongozi wa majimbo uliofanyika mjini Berlin, uliangalia pia uwezekano wa mchakato wa waomba hifadhi kufanyika nje ya bara la Ulaya, lakini scholz alilitilia shaka hilo kuona iwapo linakubalika kikatiba na iwapo mataifa mengine yataridhia.

Idadi ya waomba hifadhi yapanda maradufu ikilinganishwa na mwaka uliyopita

Ujerumani inakabiliwa na idadi kubwa ya wakimbizi
Ujerumani inakabiliwa na idadi kubwa ya wakimbiziPicha: Julian Stratenschulte/dpa/picture alliance

Makaazi ya kuwaweka wahamiaji na wakimbizi yamefurika nchini Ujerumani kwa miezi kadhaa sasa na Scholz anaepitia shinikizo kubwa kutoka kwa upinzani na kwengineko, la kusimamisha wimbi hilo la wakimbizi wanaoingia nchini humo, alisema wahamiaji wengi zaidi wataingia Ujerumani.

Idadi ya waomba hifadhi mwaka huu imepanda kwa asilimia 73 hadi mwishoni mwa mwezi Septemba ikilinganishwa na Septemba mwaka uliopita. Ujerumani pia imewapa hifadhi zaidi ya raia wa Ukraine milioni moja tangu taifa hilo lilipovamiwa kijeshi na Urusi mwezi Februari mwaka jana.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika mkutano unaofanyika nchini Uhispania katikati ya mzozo wa uhamiaji barani Ulaya

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative für Deutschland au Mbadala kwa Ujerumani, AfD, ambacho ndicho cha pili katika kura za kitaifa kikiwa mbele ya vyama vyote vitatu katika serikali ya muungano ya Scholz, ndicho chama cha kwanza kuzua wasiwasi na mjadala kuhusiana na ongezeko la wahamiaji nchini Ujerumani.

Mwezi uliopita Kansela Scholz aliliambia bunge la Ujerumani kwamba vyama vinavyozingatia demokrasia vinapaswa kuungana pamoja kutafuta muafaka juu ya wahamiaji, ili kukidhibiti chama cha AfD alichokiita chama kinachotaka uharibifu.

Chanzo: dpa/ap/reuters