1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz kukutana na wakuu wa majimbo kujadili wahamiaji

6 Novemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anakutana leo na mawaziri wakuu wa majimbo 16 yanayounda shirikisho la Ujerumani, kujadili njia za kushughulikia idadi ya wahamiaji inayoongezeka.

https://p.dw.com/p/4YTdI
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Hifadhi za wakimbizi na waomba hifadhi zinazidi kufurika na Scholz, ambaye anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa upinzani na kwingineko kukomesha mwekeleo huo, amesema watu wengi zaidi wanakuja. 

Huu ndiyo mkutano muhimu zaidi wa kilele kati ya serikali kuu na majimbo katika muda mrefu.

Kansela wa Shirikisho Olaf Scholz anakutana na wakuu wa serikali  16 za majimbo. Mada za mkutano huu ni juu ya gharama za makazina huduma kwa wakimbizi na kuzuwia uhamiaji haramu. 

Ujerumani pia imewapokea zaidi ya wakimbizi milioni moja kutoka Ukraine, tangu kuanza kwa vita vya Urusi dhidi ya nchi yao.

Soma pia:Scholz kukutana na wakuu wa majimbo kujadili wahamiaji

Mada nyingine motomoto ni ufadhili wa tiketi ya usafiri wa umma - maarufu Deutschlandticket. 

Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na msururu wa shughuli za serikali, ikiwa ni pamoja na sheria ya kurahisisha urejeshaji wa waomba hifadhi ambao maombi yao yamekataliwa, hadi kuongeza makali ya adhabu kwa wasafirishaji haramu na kuruhusu waomba hifadhi kuanza kufanya kazi mapema, na kuanzishwa kwa ukaguzi wa muda kwenye mipaka ya Polandi, Jamhuri ya Czech na Uswisi.

Scholz akabiliwa na shinikizo dhidi ya wahamiaji

Scholz, mwanasiasa wa chama cha mrengo wa wastani wa kushoto cha SPD, pia amejadili suala hilo mara mbili na kiongozi wa upinzani wa kihafidhina tangu uchaguzi wa majimbo mwezi uliopita kuleta matokeo mabaya kwa muungano wake wa vyama vitatu vinavyozozana na mafanikio kwa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD. 

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Faeser
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na waziri wa Mambo ya Ndani Nancy FaeserPicha: ANNEGRET HILSE/REUTERS

Anakabiliwa na shinikizo kuja namtokeo katika mkutano wa leona wakuu wa serikali za majimbo, wanaotaka fedha zaidi kutoka serikali ya shirikisho kumudu gharama za kuwapokea wahamiaji.

Hata hivyo uongozi wa chama kikuu cha upinzani, CDU, umetilia mashaka juu ya ufanisi wa mazunguzo ya leo, ukisema matokeo yake hayatatosha kupunguza idadi ya wahamiaji kwa njia endelevu.

Soma pia:Uhamiaji: Ujerumani yajipanga kushughulikia masuala ya wakimbizi

Waziri Mkuu wa Jimbo la North-Rhine Westphali Hendrik Wüst, alisema katika mahojiano na shirika la Utangazaji la Umma, ARD, kwamba ili kuwa na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo wahamiaji, ni lazima kukomesha uhamiaji haramu ili kuweza kuwajumuisha vyema watu wanaotafuta hifadhi nchini Ujerumani. 

Wüst alisema hatua ambazo zinaweza kusaidia ni pamoja na kuhakikisha taratibu za haraka za kupata hifadhi kwa wahamiaji kutoka nchi ambazo chini ya asilimia 5 ya waombaji hupatiwa hifadhi.

Pia aligusia wazo la kushughulikia maombi barani Afrika, jamabo ambalo linaungwa mkono na baadhi katika chama cha Scholz. 

Takribani watu 230,000 wameomba hifadhi nchini Ujerumani katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, idadi kubwa kuliko maombi jumla ya mwaka 2022. 

Serikali ya Scholz  haihitaji uungwaji mkono wa upinzani kupitisha sheriakatika bunge la wawakilishi, Bundestag, lakini inahitaji idhini ya majimbo 16 katika baraza la pili, Bundesrat, na analazimika kuzungumza na mawaziri wakuu vyama vitano tofauti. 
Kwa kuzingatia ufinyu wa bajeti na viwango vya juu vya riba, mazungumzo ya leo yanatarajiwa kuendelea mpaka usiku.
 

Ujerumani: Rasimu ya kuwarudisha watu katika mataifa yao