Ujerumani: Watu kadhaa wajeruhiwa kwenye mkutano wa Eritrea
17 Septemba 2023Mvutano wa kisiasa umeenea kati ya jamii ya taifa hilo wanaoishi uhamishoni nje ya nchi kutoka Eritrea taifa la Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser amelaani ghasia hizo zilizozuka mjini Stuttgart. Amesema migogoro ya migawanyiko ya kisiasa za nchi za kigeni haipaswi kutokea nchini Ujerumani na amesisitiza kwamba wahusika wa ghasia hizo lazima washikiliwe ili kuwajibishwa. Faeser amewatakia maafisa waliojeruhiwa afueni ya haraka.
Mapigano yalizuka wakati wa mkutano wa vyama vya Eritrea vilivyokuwa na washiriki wapatao 80 hadi 90. Jeshi la polisi, lililokuwa na askari wapatao 300 kwenye mkusanyiko huo, limeeleza kuwa wafuasi raia wa Eritrea wanaounga mkono serikasli ya rais Isaias Afwerki iliyomo madarakani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika walilumbana na mamia ya watu waliojitokeza kupinga utawala wa kiongozi huyo.
Soma:Amnesty International yavituhumu vikosi vya Eritrea kufanya ukatili Tigray
Umati huo wa takriban watu mia saba ulipewa eneo la kufanya maandamano lakini ukaliacha na kwenda mahali pa mkutano kisha wapinzani hao waliwashambulia washiriki waliokuwa kwenye mkutano pamoja na maafisa wa polisi kwa nondo, chupa, mawe na vitu vingine.
Mbali na polisi 26 waliojeruhiwa wengine ni pamoja na washiriki wanne wanaoiunga mkono serikali ya Eritrea na wanaharakati wawili wa upinzani.
Waliokimbia kutoka nchini Eritrea wamesema walifanya hivyo ili kuepuka hatari na mateso hivyo kufanywa sherehe kama hizo ni jambo ambalo limewakasirisha.
Soma: Waeritrea waelezea kupitia mateso na unyanyasaji wakati wa zoezi la huduma ya kitaifa
Eritrea imetawaliwa na Isaias Afwerki chini ya udikteta wa chama kimoja tangu mwaka 1993. Kulingana na ripoti ya Human Rights Watch Eritrea haina bunge wala mahakama pia haina mashirika huru ya kiraia au vyombo vya habari.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema Afwerki ni miongoni mwa madikteta na wakandamizaji duniani.
Vyanzo:DPA/DW