1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani huenda ikawatimua maelfu ya wahamiaji wa Nigeria

13 Novemba 2023

Mipango ya serikali ya Ujerumani ya kuongeza kasi ya kuwafukuza wahamiaji ambao maombi yao ya ukimbizi yamekataliwa, huenda ikawaathiri maelfu ya wahamiaji kutoka Nigeria.

https://p.dw.com/p/4YkP2
Mwanamke anayetembea katika kambi moja ya wakimbizi iliko Ulaya
Mwanamke anayetembea katika kambi moja ya wakimbizi iliko Ulaya Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Watu wengi wanaoishi Nigeria wamekuwa wakifuatilia kwa ukaribu mjadala mkali kuhusu masuala ya uhamiaji barani  Ulaya, hasa tangu Ujerumani ilipoidhinisha mwezi uliopita sheria ya kuiwezesha mamlaka kuwafukuza watu ambao maombi yao ya ukimbizi yamekataliwa.

Sheria iliyopendekezwa na Ujerumani huenda ikapelekea maelfu ya Wanigeria kurejeshwa nchini mwao. Licha ya azma ya Berlin ya  kuimarisha sera yake ya uhamiaji, Wanigeria wengi bado wana ndoto ya kuishi Ulaya.

Ujerumani inataka kupunguza mafao ya wakimbizi?

Mkazi mmoja wa mjini Abuja amesikika akisema kuwa ikiwa atapata fursa ya kwenda kihalali sehemu kuliko maisha bora, itakuwa vyema kwani ugumu wa maisha huko una changamoto kubwa.

Lakini Wanigeria wengine wameonyesha mashaka juu ya uamuzi ambao mara nyingi huwa hatari ya kuondoka katika nchi yao kwa lengo la kuingia barani Ulaya. Raia mmoja amesema asingependa kuondoka Nigeria huku akihoji ikiwa wote wataondoka ni nani atakaesalia nchini humo? Mwingine amesisitiza kwamba kinachohitajika ni kuiendeleza Nigeria badala ya kuondoka.

Kwa nini Wanigeria wengi hutaka kuishi Ujerumani?

Baadhi ya raia wa Nigeria mjini Lagos
Baadhi ya raia wa Nigeria mjini Lagos Picha: Emmanuel Osodi/AA/picture alliance

Nigeria, ni nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika na mojawapo ya nchi zenye demokrasia imara zaidi katika eneo la Afrika Magharibi. Lakini nchi hiyo imekuwa ikikabiliana na matatizo ya rushwa, ukosefu wa ajira, pamoja na uasi wa wanamgambo wa Kiislamu ambao umedumu kwa miaka 14 katika eneo la kaskazini mashariki, ambapo takriban watu 40,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni 2 wamekimbia makazi yao tangu mwaka 2009.

Zaidi ya maombi 1,800 ya ukimbizi yaliwasilishwa na Wanigeria kwa mamlaka ya Ujerumani kati ya Januari na Septemba mwaka huu. Judith Ibi, mwanasheria wa Nigeria, ameiambia DW kwamba Wanigeria waliowengi huondoka nchini mwao kwa matarajio ya kupata kazi iliyo bora, mishahara ya juu na hali jumla ya viwango vya maisha vilivyoboreshwa nchini Ujerumani.

Ujerumani yaridhia masharti magumu kwa wahamiaji na wakimbizi

Mwanasheria huyo anailaumu serikali ya Abuja kwa kutotekeleza jukumu na wajibu wake kwa Wanaigeria, akisema kuwa katiba ya nchi hiyo inaelezea umuhimu wa kuwepo sera za ustawi wa jamii zinazotakiwa kuidhinishwa ili kurahisisha maisha ya raia nchini Nigeria.

Scholz atoa wito wa kuwepo ushirikiano ili kudhibiti suala la uhamiaji.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Liesa Johannssen/REUTERS

Wakati wa ziara yake nchini Nigeria mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alitoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya mataifa hayo mawili ili kudhibiti suala la uhamiaji. Alielezea kuhusu ujenzi wa vituo vya kuwapokea uhamiaji ambao wanarejeshwa kutoka Ujerumani na katika nchi nyingine, huku akisisitiza kuhusu kurejea kwa wahamiaji ambao maombi yao yamekataliwa. Akiwa mjini Lagos, Scholz alisema hilo linahitaji maandalizi na uwekezaji kwa pande zote mbili.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu amesema anaunga mkono suala la kurejeshwa kwa wahamiaji hao na kwamba mikakati inaendelea ya kuongeza vituo vya uhamiaji nchini humo, lakini amesema watarejeshwa ikiwa tu itabainika kuwa ni raia wa Nigeria.

Nchi za EU zaafikiana kuhusu mkataba wa wahamiaji

Kuthibitisha hilo inaweza kuwa sehemu yenye utata na ngumu zaidi katika mpango huo, kwa sababu mara nyingi huwa vigumu kubainisha uraia wa wahamiaji hao kwa kuwa mara nyingi huwa hawana vitambulisho. Kati ya waomba hifadhi 14,000 kutoka Nigeria wanaolazimika kuondoka Ujerumani, 12,500 watalazimika kukaa zaidi Ujerumani kwa sababu hawana nyaraka zinazoweza kutambulisha uraia wao.