1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Uholanzi na Denmark kuipatia Ukraine ndege za kivita F-16

21 Agosti 2023

Ukraine itapokea zaidi ya ndege 60 za kivita chapa F-16 kutoka Uholanzi na Denmark kwa dhima ya kulisaidia jeshi la nchi hiyo kuilinda anga yake dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4VO21
Ndege za Kivita chapa F-16
Ndege za Kivita chapa F-16Picha: Gianluca Vannicelli/IPA/picture alliance

Hayo yametangazwa wakati wa ziara ya ghafla ya rais Volodomyr Zelensky kwenye mataifa hayo mawili yaliyo wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Rais Zelensky alikuwa mjini Amsterdam, Uholanzi jana Jumapili na baadaye akasafiri hadi nchini Denmark ambako kwenye mataifa hayo yote mawili alikuwa na mazungumzo na Mawaziri Wakuu.

Ziara hiyo ambayo haikutangazwa ilifuatilia ile aliyoifanya nchini Sweden siku ya Jumamosi.

Matokeo ya safari hiyo ni ahadi kutoka Uholanzi na Denmark ya kuipatia Ukraine ndege mamboleo za kivita chapa F-16.

Ndege hizo zinazoundwa na Marekani ni miongoni mwa zile zinazotumia teknolojia ya juu ya kabisa na zenye uwezo mkubwa wa kivita.

Uholanzi kutoa ndege 42 na Denmark ndege 19

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rute amesema nchi yake itatoa ndege 42 zitakazopelekwa Ukraine baada ya marubani wa nchi hiyo kukamilisha mafunzo ya kuzirusha.

Tarehe kamili ya kupelekwa ndege hizo za Uholanzi bado haijawekwa wazi. Alau kwa sasa ni ndege 24 tu kati ya 42 za taifa hilo ndiyo zinafanya kazi.

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine pamoja na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen
Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine pamoja na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen Picha: Mads Claus Rasmussen/REUTERS

Baada ya kutumia saa chache nchini Uholanzi, rais Zelensky alielekea Denmark alikopokea ahadi nyingine ya kupatiwa aina hiyo ya ndege kutoka kwa Waziri Mkuu wa taifa hilo Mette Frederiksen kama msaada wa ziada katika vita vinavyoendelea

"Tunafahamu mnayo mahitaji makubwa, na ndiyo maana leo tunatoa ndege 19 chapa F-16 kwa Ukraine. Pamoja na Uholanzi, tunakuwa nchi ya kwanza kutoa ahadi ya uhakika ya kukupatieni ndege za kivita kutoka mataifa ya magharibi na tuna matumaini wengine watafuata" alisema Waziri Mkuu Mette.

Duru zinasema sehemu ya ndege hizo za Denmark zitapelekwa Ukraine kabla ya mwishoni mwa mwaka 2023.

Zelensky asifu uamuzi huo lakini Urusi itajibu vipi hatua hiyo?

Kwa miezi kadhaa sasa rais Zelensky amekuwa akitoa rai kwa mataifa washirika ya magharibi kulipatia jeshi lake msaada wa ndege za kisasa za kivita hususani F-16 kuliwezesha kuilinda kikamilifu anga ya nchi hiyo.

Niederlande | Wolodymyr Selenskyj besichtigt F-16 Kampfjets
Rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky pamoja na Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte wakitembelea karibu na ndege chapa F-16 huko Eindhoven, Uholanzi. Picha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Hata hivyo Marekani, iliweka kizingiti kwa taifa lolote kuipatia Ukraine aina hiyo ya ndege ikihofia kuutanua mzozo unaoendelea.

Ni siku chache pekee zimepita ndiyo serikali ya Washington iliondoa zuio lake na kuruhusu nchi yoyote inayoweza kuipatia Ukraine aina hiyo ya ndege basi mlango uko wazi.

Na kwa hakika ahadi za Uholanzi na Denmark zimemfurahisha sana rais Zelensky.

"Leo kumetolewa ishara ya maana kubwa hususani kwamba kila mmoja atafanya lililo ndani ya uwezo kuhakikisha tunapata ndege za kwanza haraka iwezekanavyo. Sihitaji kugusia suala la tarehe (ya ndege kutumwa) , lakini pameoneshwa ishara muhimu sana" amesema kiongozi huyo.

Urusi kwa upande wake bado haijasema juu ya tangazo hilo la Ukraine kupatiwa ndege za kisasa.

Lakini mnamo mwezi uliopita Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov alisemanchi yake itazingatia kuwa imo katikati ya kitisho cha nyuklia iwapo mataifa ya magharibi yataipatia Ukraine ndege chapa F16.

Lavrov alisema pindi washirika wa Ukraine watafikia uamuzi kutoa msaada wa aina hiyo kwa Ukraine, Urusi haitapuuza uwezo wa ndege hizo kubeba silaha za nyuklia na kwa hivyo Moscow italizingatia hilo kuwa kitisho cha  wazi cha nyuklia.